Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wasichana chini ya Umri wa miaka 17 ‘Serengeri Girls’ Bakari Shime, amekiri kufurahishwa na maendeleo ya kikosi chake kinachojiandaa na Fainali za Kombe la Dunia zitakazounguruma Oktoba 11-30 nchini India.

Kikosi hicho kimeweka Kambi kisiwani Unguja ‘Zanzibar’, kujiandaa na Michuano hiyo ambayo Tanzania itashiriki kwa mara ya kwanza, baada ya kufuzu ikitokea Barani Afrika ambako ilizifunga timu za taifa za Cameroon, Botswana na Burundi.

Kocha Shime amesema wachezaji wake wamekua na uelewa mkubwa tangu walipoanza kambi visiwani humo, ana uhakika wa kwenda kwenye Fainali za Kombe la Dunia na kuonyesha upinzani mkubwa.

Amesema amedhamiria kuweka rekodi ya kipekee katika Fainali hizo, kutokana na Wachezaji wake kuonesha utayari wa kwenda kupambana bila kuchoka.

“Tumejipanga vizuri tunataka tuishangaze Dunia kwa kuonesha kiwango bora katika mashindano haya, ikiwezekana tuwe mabingwa.” amesema Bakari Shime

Kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2022, Serengeti Girls imepangwa Kundi D Sambamba na nchi za Japan, Canada na Ufaransa.

Timu hiyo itaanza kusaka ubingwa wa Dunia kwa kucheza na Japan Oktoba 12 , kisha itacheza dhidi ya Ufaransa Oktoba 15 na kumaliza hatua ya Makundi kwa kupapatuana na Canada mnamo Oktoba 18.

Michezo ya Kundi D imepangwa kuchezwa katika Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru, uliopo mjini Margao.

Makamba: "Sasa kazi ni usiku na mchana ujenzi Bwawa la Nyerere"
Kenya: Hitilafu zasababisha uchaguzi kuahirishwa