Kocha Mkuu wa Geita Gold FC, Fred Felix Minziro amesema wanahitaji alama tatu dhidi ya Mabingwa watetezi Young Africans kwenye mchezo wao ujao wa ligi ambao utapigwa kesho Jumapili (machi 12) kwenye Dimba la Azam Complex, Dar.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Minziro amesema kuwa wanatambua wapinzani wao wamejipanga kutetea ubingwa kwa kuhakikisha wanapambana kwenye mchezo wa kesho, lakini hata kwa upande wake amejipanga kupata matokeo mazuri ugenini.

“Tumekuja Dar es salaam na wachezaji 22 wote wapo vizuri na wapo tayari kwa mchezo wetu ujao ambao ni muhimu na utakuwa na ushindani mkubwa nasi tunahitaji kupata matokeo mazuri.”

“Inabidi hufahamu kwamba tunacheza na Young Africans, ambao wao wanapambania kutetea ubingwa, sisi tumekuja hapa kupambana kwa ajili ya kupata matokeo.”

“Uwanja ambao tutatumia ni ule wa kapeti na tutatumia kufanya maandalizi kwa kutumia Uwanja wa Uhuru ambao ni wa kapeti hivyo hilo litatufanya tuweze kuzoea mazingira ya uwanja tutakaotumia.”

“Tuna mchezo mmoja ugenini kisha baada ya hapo tutarudi kwa ajili ya mchezo mwingine nyumbani hilo limefanya tukachagua idadi ya hawa wachezaji ambao tupo nao hapa Dar es salaam,” amesema Minziro

Geita Gold FC inajiandaa kukutana na Young Africans ikiwa nafasi ya 05 kwa kufikisha alama 34, huku wenyeji wao Young Africans wakiwa kileleni kwa kumiliki alama 64.

Robertinho atenga siku tisa kuimaliza Horoya AC
Wizara kushirikiana na ATE usimamizi sheria za kazi, ajira