Kocha Mkuu wa AS Vita Club Frolent Ibenge ameonyesha hofu dhidi ya wapinznai wake Simba SC kutoka Tanzania, ambao kesho Ijumaa (Februari 12) atakabiliana nao kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi A wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Ibenge ambaye pia ni kocha mkuu wa timu ya taifa ya DR Congo, amesema Simba SC imeendelea kuwa klabu ya kipekee katika klabu ambazo aliwahi kukutana nazo katika ushindani wa kimataifa.

Amesema anakwenda kukabiliana na Simba SC ambayo bado ina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa wa kupambana, huku akikiri kuwakumbuka baadhi yao ambao walikuwepo kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa Barani Afrika msimu wa 2018/19.

Amesema wachezaji kama Clatous Chama na Jonas Mkude ni sehemu ya watu anaowakumbuka, hivyo anabudi kujihadhari kuelekea mchezo wa kesho ambao utaanza majira ya saa nne kwa saa za Afrika Mashariki.

“Nawakumbuka wachezaji wengi wazuri ndani ya kikosi cha Simba kama Clatous Chama na Jonas Mkude, kwenye mchezo wetu wa mwisho dhidi yao ambao tulipoteza, nakumbuka Chama ndiye alitufunga bao lililotutoa kwenye mashindano.“

“Lakini pia namkumbuka Mkude alicheza vizuri, nadhani wachezaji hao wanahitaji ulinzi zaidi ili wasitupe madhara kuelekea mchezo huu ambao tutakuwa nyumbani.”

“Mchezo huu ni tafsiri halisi ya mpira, lazima ukutane na mpinzani ambaye unahisi kuwa atakupa changamoto, na unatakiwa uwe tayari kuzikabili changamoto hizo.“

“Nadhani wapinzani wetu hawatakuwa tayari kufungwa mabao mengi kama ilivyotokea awali walipokuja Congo,” amesema Frolent Ibenge.

Simba SC tayari imeshawasili mjini Kinshasa, Dr Congo na jana usiku iliendelea na mazoezi ikiwa mjini humo, tayari kwa mchezo dhidi ya AS Vita Club, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini Tanzania.

Mahusiano Tanzania, Saudi Arabia yazidi kuchanua
Magufuli akerwa na 'uozo' soko la Morogoro