Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya DR Congo Frolent Ibenge, ametegua kitendawili cha kutua kwa mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC, ambao wanamsaka mbadala wa kocha Sven Vanderbroeck alieachana na klabu hiyo juma lililopita.

Ibenge ametegua kitendwili hicho alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, baada ya kushuhudia kikosi chake kikilazimishwa sare ya bao moja kwa moja dhidi ya timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), jana Jumatano Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kocha huyo kutoka DR Congo amesema anafahamu uongozi wa Simba SC unamfuatilia katika kipindi hiki ambacho wanamsaka mbadala wa kocha Sven, na anatambua ukubwa na umuhimu wa klabu hiyo katika soka la ndani na nje ya Tanzania.

Hata hivyo Ibenge amesema kwa sasa yeye ni kocha wa AS VITA ya nchini kwao DR Congo na kama kutakua na mabadiliko ulimwengu wa soka utalifahamu suala hilo.

“Simba ni timu kubwa na yenye ushindani ndani ya Ligi Kuu Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika, hilo siwezi kukataa.”

“Ninajua kwamba wanahitaji huduma yangu hilo lipo wazi hata msimu uliopita walinihitaji lakini shida ni kuwa kwa sasa mimi ni mwalimu wa AS Vita na Congo.

“Kama ningekuwa sina timu basi ningesema itakuaje lakini kwa sasa tusubiri na tuone bado nipo DR Congo na timu yangu ya AS Vita,” amesema Ibenge.

Kocha Ibenge amekua sehemu ya makocha wanaotajwa kuwania na Simba SC, huku akipewa kipaumbele kikubwa cha kutua Msimbazi kuendeleza mipango na mikakati iliyoachwa na kocha Sven Vanderbroeck aliyetimkia F.A.R ya Morocco.

Waziri: Wadaiwa katika ranchi kukiona
Songne hatarini kuikosa Simba SC