Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amesema ameanza kuifuatilia Primeiro de Agosto ya Angola kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza Mzunguuko wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Simba SC itaanzia ugenini nchini Angola Oktoba 08, na juma moja baadae itamalizia nyumbani Dar es salaam Uwanja wa Benjamin Mkapa Oktoba 16.

Kocha Mgunda amesema amegundua mambo mengi ya kiufundi kuhusu wapinzani wao, lakini kikubwa amejifunza kuwa Primeiro de Agosto ni timu inayopambana kwa nguvu na wachezaji wake wanatumia akili nyingi muda wote.

Amesema kutokana na hilo, hana budi kukiandaa kikosi chake kutokana na uhalisia aliouona kwa wapinzani wao, na anaamini mpambano utakawa na upinznai mkubwa.

“Primeiro de Agosto ni timu inayotumia nguvu na wachezaji wake wapo timamu, hivyo hatutakuwa na ulazima wa kucheza kama wanavyocheza wao, kazi kubwa iliyopo mbele yetu ni kuhakikisha tunaandaa kikosi ambacho kitacheza kiakili zaidi ili kukwepa kutolewa mchezoni,” amesema Mgunda

Amesema kikubwa watakachokifanya katika mchezo huo wa awali ugenini ni kucheza mchezo wao na si kuiga wa wapinzani wao ambao watakuwa uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki wao.

Primeiro de Agosto msimu huu inaelezwa kufanya usajili mkubwa, kikosi chake kikiundwa na wachezaji kutoka mataifa mbalimbali ikiwamo Ureno na Brazil na imefanya vizuri katika mchezo wake wa awali kwa kuitoa Red Arrows ya Zambia kwa jumla ya mabao 2-1 ikishinda bao 1-0 ugenini na nyumbani kutoka sare ya 1-1.

Lakini hilo si tatizo kubwa kwa Simba, kwani yenyewe ilipata ushindi mkubwa ugenini wa mabao 2-0 na kama huo nyumbani hivyo kuitoa Nyasa Big Bullets ya Malawi kwa jumla ya mabao 2-0.

Tayari mshambuliaji hatari wa Simba, Moses Phiri, ametoa ahadi ya kuendelea kushirikiana vema na wachezaji wenzake kuipambania timu yao kuweza kufika mbali kwenye michuano hiyo msimu huu.

Phiri hadi sasa ana mabao matatu mkononi kwenye michuano hiyo baada ya kufunga moja ugenini dhidi ya Nyasa Big Bullets na kisha kutupia yote mawili wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 2-0 Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Simba ambayo ipo Zanzibar bila kikosi chake kamili, kutokana na baadhi kuwa katika timu zao za taifa kipindi hiki cha Kalenda ya Fifa, baada ya kuivaa Kipanga FC keshokutwa, itarejea Dar es Salaam na kisha Oktoba 2, mwaka huu itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza mechi moja ya Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji FC kabla ya kuifuata Primeiro de Agosto.

Hersi Said kumaliza tofauti Young Africans
Waandamanaji 'kifo cha Hijab' wateka mji, 35 wauawa