Chama cha soka nchini Uholanzi KNVB, usiku wa kuamkia leo kilithibitisha taarifa za kujiuzulu kwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo Guus Hiddink.

Hiddink mwenye umri wa miaka 68, ameripotiwa kuachia ngazi kutokana na hali inavyomuendea kombo katika harakati za kuiwezesha timu ya taifa ya Uholanzi kufuzu kucheza fainali za mataifa ya barani Ulaya za mwaka 2016 ambazo zitafanyika nchini Ufaransa.

Barua aliyoiwasilisha kwa mabosi wake, inadaiwa kuwa na maelezo ya kukubaliwa na hali ngumu katika utendaji wake wa kazi na ameona ni bora ajiweke pembeni kabla ya kuishuhudia Uholanzi ikipoteza muelekeo wa kushindwa kuelekea nchini Ufaransa mwakani.

Tayari KNVB wameshamthibitisha kocha msaidizi Danny Blind, kuchukua madaraka ya kukiongoza kikosi cha timu ya taifa ya Uholanzi katika kampeni za kusaka nafasi ya kufuzu kwenye fainali za barani Ulaya za mwaka 2016.

Kuna hatari kwa timu ya taifa ya Uholanzi kucheza mchezo wa mtoano ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu kwenye fainali za barani Ulaya, kufuatia kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi la kwanza ambalo linaongozwa na Iceland.

Tofauti ya point tano dhidi ya vinara wa kundi hilo zinaendelea kuwapa wakati mgumu viongozi wa chama cha soka pamoja na wale wa benchi la ufundi na ndipo Hiddink alipoona ni bora ajiweke pembeni kwa kuamini huenda mbadala wake akafanikiwa kufaulu mtihani wa kuivusha Uholanzi.

Hiddink alikishuhudia kikosi chake kikipoteza mchezo wa kundi la kwanza dhidi ya Czech Republic pamoja na Iceland mwezi Septemba pamoja na Oktoba mwaka 2014 huku wakishindwa katika mchezo mwingine muhimu mbele ya Uturuki katika uwanja wa nyumbani.

Huenda katika kipindi hiki ikiwa si bahati kwa Hiddink, ikilinganishwa na kipindi cha nyuma alipokuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uholanzi ambapo alifanikisha safari ya kuwawezesha The Orange kufika kwenye hatua ya nusu fainali wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 1998 kule nchini Ufaransa.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa kikosi cha Uholanzi ambacho kilikuwa kikiongozwa na meneja wa klabu ya Man Utd, Louis Van Gaal, kilifanikiwa kufika katika hatua ya nusu fainali wakati wa fainali za kombe la dunia zilizofanyika nchini Brazil mwaka 2014.

Picha: Ali Kiba Apangiwa Staa wa Kike Ndani ya Coke Studio Africa
January Makamba: CCM impitishe kijana atakayeleta mabadiliko