Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar Salum Shaban Mayanga amewapongeza wachezaji wake kwa kazi kubwa walioifanya dhidi ya Tanzania Prisons na kufanikiwa kubaki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu ujao.

Mtibwa Sugar imebaki Ligi Kuu kwa kupata ushindi wa jumla wa 3-2, baada ya kucheza michezo miwili ya hatua ya mtoano (Play Off), katika viwanja wa Sokoine (Mbeya) na Manungu Complex (Morogoro).

Mayanga amesema haikuwa rahisi kwa wachezaji wake kupambana katika michezo hiyo, lakini kikubwa wameipambania timu yao na kufikia lengo walilojiwekea baada ya kujikuta wameangukia kwenye michezo ya Play Off.

“Ninawapongeza sana wachezaji wangu kwa kazi nzuri walioifanya, kwa hakika haikuwa rahisi kufikia hili, kupambana kwao ndio imekua furaha kwa Wanamtibwa wote, kilichobaki ni kuangalia namna ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ili tuweze kushiriki vizuri na tusirudie makossa yaliyotufikisha  kwenye ‘Play Off’ kwa msimu wa 2021/22.”

“Nitakaa chini na viongozi na kuwashauri masuala ya kiufundi ili kuongeza nguvu katika maeneo machache kwenye kikosi chetu, nina imani tutafanikiwa katika hili kutokana na makosa ambayo yamekua yakijirudia mara kwa mara” amesema Mayanga

Mtibwa Sugar imecheza mchezo wa Play Off kwa msimu wa pili mfululizo, kufuatia kikosi chao kutokua na matokeo mazuri katika michezo ya Ligi Kuu na kujikuta kikiangukia kwenye kapu hilo.

Patrick Odhiambo: Tuna kazi ya kufanya JKT Tanzania
Mwinyi mgeni rasmi maadhimisho siku ya Kiswahili Duniani