Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Mohamed Nabi amesema mchezo wa kesho Jumatano (Juni 29) dhidi ya Mtibwa Sugar, hautakua rahisi kama Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo wanavyotarajia.

Young African itakua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa kupepetana na Mtibwa Sugar katika mchezo huo wa mwisho wa Ligi Kuu msimu huu 2021/22, huku ikiwa klabu pekee ambayo haijapoteza mchezo hadi sasa.

Kocha Nabi amezungumza na Waandishi wa Habari leo mchana (Juni 28) jijini Dar es salaam na kuweka wazi namna anavyoutazama mchezo huo ambao anatarajia kuona mashabiki wengi wakifika Uwanja wa Mkapa kuishangilia timu yao.

“Hautakua mchezo rahisi kama inavyofikiriwa, nina uhakika huu ndio mchezo mgumu kuliko yote tuliocheza kwa msimu huu, kwa sababu Mtibwa Sugar kuifunga Young Africans itakua ni faida kwao kutokushuka Daraja, na Young Africans haitakua tayari kuchafuliwa rekodi yake ya kutopoteza mchezo msimu huu.”

“Wachezaji wangu kama wanane hawatakuwa sehemu ya kikosi changu kesho kutokana na sababu mbalimbali (wanatumikia adhabu ya kadi za njano), hii inatupa wakati mgumu wa kuamini hautakua mchezo rahisi.”

“Ifahamike kuwa baada ya siku tatu tutakua na mchezo wa Fainali ya ASFC, pia hii inanipa wakati mgumu wa kupanga kikosi ili niweze kuwa na kikosi imara katika mchezo wa Fainali dhidi ya Coastal Union.” Amesema Nabi

Wachezaji Young Africans wapigwa marufuku Ubingwa Ligi Kuu
Sabasaba 2022 kampuni za nje zaongeza ushiriki