Licha ya kuibanjua Simba SC bao 1-0 na kikosi chake kuonesha soka safi katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, amesema bado ana kazi kubwa ya kufanya ili kupata muunganiko mzuri wa kikosi chake.

Kocha Nabi amesema anaendelea kupambana ili kufanikisha jambo hilo, huku akiamini endapo atafanikiwa katika hilo kikosi chake kitakua na makali ya kutisha katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao unaanza rasmi leo Jumatatu (Septemba 27).

Kocha huyo kutoka nchini Tunisia ameongeza kuwa hana shaka na wachezaji wake hasa waliosajiliwa msimu huu, lakini akaendelea kusisitiza kuwa, atapambana ili kufanikisha azma ya kupata muunganiko.

“Usajili tu hapo siwezi kudanganya ni usajili mzuri umefanywa na viongozi na mimi nimehusika kwa kuwa nipo kwenye kamati ya usajili lakini suala la muunganiko hilo bado halijawa sawa.

“Nikiwa ni mwalimu wa mpira ambaye ninapenda kuona matokeo ninaweka wazi kuwa itachukua zaidi ya wiki mbili na pengine zaidi ya hapo lakini haina maana kwamba tutashindwa kushinda hapana tutafanya vizuri na kila kitu kitakuwa sawa,” amesema Nabi.

Young Africans kwa sasa ipo kwenye maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Kaitaba keshokutwa Jumatano (Septamba 29).

Makamba: TANESCO iendeshwe kibiashara
Simba SC yatangaza njaa 2021/22