Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Ethiopia Klabu ya St. George, Zerihun Shengeta ameukubali Mziki wa Simba SC, baada ya kukishuhudia kikosi chake kikilala kwa Mkapa kwa kukubali kufungwa 2-0 jana Jumapili (Agosti 08).

St George ilialikwa kucheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Simba SC, ikiwa ni sehemu ya kusherehesha Tamasha wa Simba Day, lililofanyika kwa mafanikio makubwa mwaka huu 2022, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kocha Shengeta amesema licha ya kikosi chake kuonesha upinzani wa kutosha dhidi ya Simba SC, lakini bado kilizidiwa mbinu nyingi na kujkuta kikipoteza mchezo huo ambao amekiri ulikua mzuri kwa kila upande.

Amesema kwa matokeo hayo, amejiridhisha kuwa Simba SC imeimarika na ina kikosi bora kama alivyokua akisikia kwa miaka ya hivi karibuni, kutokana na kufanya vizuri kwenye michuano ya Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

“Ulikuwa mchezo mgumu na mzuri. Soka la Tanzania limebadilika sana, nimekutana mara nyingi na Simba SC lakini kwa sasa wamebadilika sana.”

“Wana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi na kushambulia. Wana wachezaji wengi wazuri eneo la kati na pembeni.. wakielewana zaidi, watatengeneza timu nzuri Afrika.”

“Niwashukuru kunipa kipimo kizuri, pia kama timu kupata heshima ya kualikwa katika tamasha kubwa na zuri kama hili.” amesema Kocha Zerihun Shengeta

Simba SC iliyokua imeweka Kambi mjini Ismailia-Misri kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa 2022/23, itakutana na Young Africans Jumamosi (Agosti 13) Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii, ambao pia utatumika kama sehemu ya Ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Naibu Rais Ruto apiga kura akiwa na mkewe
Simba SC yaachana na Hassan Dilunga