Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Sven Vandenbroeck amesema amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake wakati wa mchezo wa mzunguuko wa 37 dhidi ya Coastal Union jijini Tanga juzi Al-Khamis.

Mchezo huo uliokua na upinzani mkali kwa dakika zote 90, ulimalizika kwa matokeo ya sare ya bila kufungana na kuifanya Simba kufikisha alama 85 kwenye msimamo wa Ligi kuu, huku Coastal Union wakifikisha alama 53 zinazowaweka nafasi ya 6.

Kocha Sven amesema kiwango cha kikosi chake kilichoonekana katika mpambano huo, kimeendelea kumdhihirishia kuwa, mipango ya maandalizi kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Namungo FC, inakwenda vizuri.

Kabla ya mchezo huo wa fainali, mabingwa Simba watashuka dimbani kesho Jumapili kumaliza Mchaka Mchaka wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika mjini Moshi.

Kocha Sven ameongeza kuwa mchezo dhidi ya Coastal Union ulikuwa na ushindani wakati wote na ilidhihirisha kila upande unahitaji ushindi ili kulinda heshima baada ya kutobadilisha malengo.

Amesema kwa hakika mpambano huo umekisaidia kikosi chake kujiimarisha kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe La Shirikisho (ASFC) na anatarajia kuona wanaendelea kucheza katika kiwango cha juu kesho na hatimaye kumaliza msimu kwa furaha.

“Ulikuwa mchezo wenye ushindani kutoka kila upande, ingawa tulistahili ushindi, natumaini tutakuwa katika kiwango bora zaidi kesho Jumapili na baadaye kwenye fainali ya ASFC, ” alisema kwa kifupi kocha huyo kutoka Ubelgiji.

Mkapa kuagwa siku tatu uwanja wa Taifa
ISIS watumia ‘lockdown’ kujiunda tena, wapanga mashambulizi nchi hizi