Kocha mkuu wa klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC Sven Vandenbroeck amefurahishwa na jinsi kikosi chake kilivyocheza dhidi ya Polisi Tanzania kwenye mchezo wa Ligi Kuu jana usiku (Desemba 09), Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Kwenye mchezo huo uliokua na upinzani wa kweli, Simba SC walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri yaliyofungwa na kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama, kipindi cha pili akiingia kuchukua nafasi ya kiungo kutoka Kenya Francis Kahata. Bao la kwanza kwa Simba lilipatikana dakika ya 65 huku bao la pili likifungwa dakika ya 90.

Kocha Sven alizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo na kusema, kwa ujumla kikosi chake kilimiliki mpira kwa kiasi kikubwa na tatizo la kubadilisha nafasi kuwa mabao liliwakabili katika kipindi cha kwanza, lakini hakuwa na shaka na hilo.

Amesema kipindi cha pili alifanya maamuzi ya kuwabadilisha baadhi ya wachezaji na kufanikiwa kupata matokeo yaliyoisaidia timu yake kuongeza alama tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, kwa kufiksha alama 26.

Francis Kahata, Bernard Morrison na Muzamireu Yassin walitolewa na nafasi zao kuchukuliwa na John Bocco, Clatous Chama na Erasto Nyoni.

“Nadhani kwa ujumla tulimiliki sana mpira na mwisho wa mchezo tumeshinda huu mchezo  mgumu. Ukiangalia Polisi hawajafungwa magoli mengi  lakini tumeweza kufunga magoli mawili na kutengeneza nafasi nyingi. Nimeridhishwa na kila mmoja.” Alisema Sven.

Baada ya mchezo huo Simba SC wanaanza safari ya kuelekea jijini Mbeya, tayari kwa kuwavaa Mbeya City kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mwishoni mwa juma hili.

Simba SC inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikitanguliwa na Azam FC walio nafasi ya pili kwa kufikisha alama 27, huku Young Africans wakiongoza msimamo huo kwa kumiliki alama 34.

Aliyenunua gari la milioni 400 asimamishwa kazi
Ghana: Mahama atahadharisha kuhusu wizi wa kura