Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wameahidi furaha kwa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo, kuelekea mpambano wao dhidi ya Namungo FC utakaopigwa Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa mkoani Lindi leo jioni.

Klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es salaam tayari ilishatangazwa kuwa mabingwa kwa msimu wa tatu mfululizo na leo baada ya mchezo dhidi ya Namungo FC itakabidhiwa kombe lao ambalo watalichukua moja kwa moja.

Simba itashuka katika mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha bao 1-0 walichopokea kutoka kwa Kagera Sugar wakati wakikabidhiwa kombe la msimu wa 2017/18, wakiwa mbele ya Rais, John Magufuli.

Namungo FC ambao wanashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza wataingia dimbani wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa magoli 3-2 na mabingwa hao walipokutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza jijini, Dar es Salaam, lakini kikosi hicho cha Kocha Mkuu, Hitimana Thiery, hakijapoteza mechi yoyote, kati ya michezo 17 iliyopita ya ligi hiyo pamoja na michuano ya Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC).

Kocha Mkuu wa Simba, Sven  Vandenbroeck, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo na wamejipanga kupata ushindi ili kutoharibu sherehe za kukabidhiwa kikombe.

Sven amesema kila mchezaji yuko tayari na amewataka kuongeza umakini ili watimize malengo yao ya kufanya vizuri zaidi msimu huu.

“Tuko tayari kwa mechi, najua haitakuwa rahisi kutokana na wenyeji kuwa na timu nzuri pia, wanacheza kwa kasi na wanauzoefu pia na mechi kubwa, wana rekodi nzuri kama ambavyo sisi tunahitaji kuweka rekodi yetu, natumaini itakuwa mechi yenye kuvutia pia,” alisema Mbelgiji huyo.

Nahodha wa timu hiyo, John Bocco amesema kila mchezo kwao ni muhimu na wataingia uwanjani kusaka ushindi bila kujali wameshakamilisha hesabu za ubingwa.

“Tuko imara na tayari kwa mechi, hakuna mechi rahisi katika ligi, sisi ni mabingwa, lakini haimaanishi tutaingia uwanjani kukamilisha ratiba, tunataka ushindi wa kupokelea kikombe,” Bocco alisema.

Michezo mingine ya mzunguuko wa 34 wa ligi kuu inayochezwa leo Jumatano Julai 08 ni kati ya Kagera Sugar dhidi ya Young Africans, Azam FC wataikaribisha Mwadui FC, Mbao vs Mtibwa Sugar, Ndanda vs JKT Tanzania, Alliance vs Lipuli, Mbeya City vs Polisi Tanzania, Biashara United vs Ruvu Shooting na KMC watawakaribisha Singida United.

Mzunguuko wa 34 wa ligi hiyo itakamilika kesho kwa Tanzania Prisons kuwakaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya.

Joshua Nassari ajiunga na CCM, azungumzia mpango wa ubunge
Singida Utd kupambana hadi mwisho