Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC, Sven Vandenbroeck anatarajiwa kurejea nchini kwa ajili ya kushiriki kongamano la soka linalotarajiwa kufanyika Machi 18 na 19, mwaka huu kwenye Ukimbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Sven ambaye ni raia wa Ubelgiji alitangaza kuachana na Simba hivi karibuni na sasa amejiunga na klabu ya FAR Rabat ya Morocco.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Afrisoccer, Peter Simon, amesema maandalizi ya kongamano hilo yamekamilika na linatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa soka kutoka nchi mbalimbali akiwamo kocha huyo wa zamani wa Simba SC.

Simon amewataja baadhi ya wageni wengine waliothibitisha kuhudhuria kongamano hilo ni pamoja na mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Senegal, Khalilou Fadida ambaye aliwahi kuichezea klabu ya Bolton Wanderers na Inter Milan, Marcos Pelegrín kutoka Afrika Kusini ambaye ni Mwakilishi wa Laliga na Mshauri wa Yanga, Senzo Mbatha.

Wengine watakaoshiriki ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, Mulamu Nghambi ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Simba, Abdulkarim Amin ‘Popat’ kutoka Azam FC na Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Wanawake Tanzania (TWFA), Amina Karuma.

Kongamano hilo litasaidia wadau wa hapa nchini kujifunza mbinu mpya za uendeshaji wa soka kupitia kwa wageni ambao nchi zao zimepiga hatua katika mchezo huo.

Chuo Kikuu cha SAUT kuzindua SAUT Alumni
Rais Magufuli kufanya ziara ya siku tatu Dar es Salaam