Kocha wa bondia Mfilipino, Manny Pacquiao anayefahamika kwa jina la Freddie Roach ameweka wazi kuwa alitembelewa hivi karibuni na Floyd Mayweather katika jumba la mafunzo la Pacquiao lililoko Hollywood, Marekani na kumkabidhi moja kati ya silaha za mafunzo za mwanafunzi wake aliyoikataa.

Roach ambaye ni bondia wa zamani anayemfahamu Mayweather tangu alipokuwa mtoto alieleza kuwa bondia huyo amekuwa akitembelea ‘gym’ ya Pacquiao iliyoko Hollywood kwa mara ya pili mwaka huu na wakati mmoja aliweza kuzungumza naye.

Alisema kuwa alimkabidhi kifaa cha mafunzo cha kuongeza kasi ya kurusha masumbwi maarufu kama ‘Speed Bag’, chenye sura yake [sura ya Mayweather] ambacho awali kiliandaliwa kwa ajili ya Pacquiao kwa ajili ya kufanyia mafunzo ya mwisho kabla hajapambana naye Mei 2 mwaka jana.

Speed Bag

Kocha huyo alisema kuwa Pacquiao alikataa kutumia speed bag hiyo yenye sura ya Mayweather kwa heshima ya bondia huyo ambaye hajawahi kushindwa hata pambano moja.

“Nilimpa Mayweather hiyo speed bag, nilifikiri ataipenda. Kweli aliipenda kwahiyo nikamkabidhi. Tuliongea kidogo lakini sio kuhusu pambano. Hata neno moja kuhusu pambano hatukuzungumzia,” alisema Roach.

Roach anaamini kuwa kutokana na tabia ya hivi karibuni ya Mayweather kupenda kutembelea gym ya Pacquiao, kuna uwezekano mkubwa wakutokea pambano la marudiano kati yao ingawa hivi sasa wote wamesema wamestaafu masumbwi.

“Ni nyumbani kwake hapa sasa, na hii inaweza kuwa gym pekee ambayo anaifahamu hapa. Lakini inavutia. Ninaendelea kusubiri nisikie anazungumzia pambano la marudiano na Pacquiao lakini hajafanya hivi. Kwahiyo na mimi sizungumzii,” alisema Mzee Roach ambaye ni mbabe wa ulingoni wa zamani.

Alisema kuwa alishawasikia Pacquiao na Meneja wake wakizungumzia kuhusu utayari na nia ya kuwepo kwa pambano la marudiano (Mayweather – Pacquiao II). Kinachosubiriwa ni neno kutoka upande wa Mayweather.

Ingawa Pacquiao ameshinda nafasi ya Useneta nchini kwake, kocha mwingine wa Pacquiao, Justin Fortune ameeleza kuwa bondia huyo atarudi ulingoni kwa ajili ya kupata fedha nyingi za kuwasaidia watu wa Ufilipino alioahidi kuwatumikia kwa moyo.

Alisema Pacquiao tayari ana fedha nyingi za kumtosha yeye na familia yake, lakini akipanda ulingoni kwa mara nyingine dhidi ya Mayweather atakuwa na sababu kama Seneta kuwatafutia fedha wananchi wake ili ziweze kuwasaidia katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

Video: Magazeti Leo May 26 2016
Video: Mbunge wa Mikumi Joseph Haule(Profesa Jay) afikisha kilio cha Mikumi Bungeni

Comments

comments