Kocha wa Senegal, Aliou Cisse ambaye alikuwa nahodha wa kikosi cha nchi hiyo mwaka 2002 amesema kuwa anaamini siku moja timu ya Afrika itashinda kombe la dunia licha ya kuanza vibaya kwenye fainali za mwaka huu.

Cisse ambaye amewahi kuchezea klabu za Birmingham City na Portsmouth, ndiye kocha pekee wa Afrika aliyeshuhudia timu yake ikianza kwa ushindi kwenye kundi lake baada ya kuipiga Poland 2-1.

“Nina uhakika kwamba ipo siku moja timu ya Afrika, nchi ya Afrika itashinda kombe la dunia,” alisema Cisse.

Hata hivyo, kocha huyo alikiri kuwa kutokana na kuanza vibaya kwa timu za Afrika kwenye fainali hizi msako wa ushindi wa kombe hilo unaweza kuchukua miaka kadhaa.

Alisema kuwa kukamilisha ndoto hii kwa timu za Afrika ni vigumu kwa kulinganisha na timu za mabara mengine kutokana na changamoto ya bajeti (fedha), miundombinu pamoja na matatizo ya mashirikisho ya nchi hizo.

Jana usiku matumaini ya Misri, mabingwa mara kadhaa wa kombe la Afrika yalififia baada ya kufungwa na wenyeji Urusi 3-1, kipigo kilichotonesha kidonda cha kipigo cha awali cha 0-1 dhidi ya Uruguay.

Wagonjwa 11 wafanyiwa upasuaji wa Moyo JKCI
Video: Mashabiki wa rapa aliyeuawa wafunga mitaa kwa fujo