Wachezaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Fiston Kalala Mayele wanainyima usingizi Zalan FC kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa Hatua ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, utakaopigwa kesho Jumamosi (Septemba 16).

Miamba hiyo itakuatana Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku Young Africans ikiwa na mtaji wa mabao 4-0, walioyapata kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa mwishoni mwa juma lililopita.

Akiwa katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo Ijumaa (Septemba 16) majira ya Mchana, Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Sudan Kusini Zalan FC Mawein Deng, amesema wachezaji hao wamekua wakiwapa wakati mgumu tangu walipocheza na Young Africans mwishoni mwa juma lililopita.

Hata hivyo Kocha huyo amesema kikosi chake kimeyafanyia kazi makosa walioyafanya kwenye mchezo uliopita na wamejiandaa vizuri kwa mchezo wa kesho, ambao utaamua hatma yao ya kuendelea ama kuondolewa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.

“Tunatarajia mchezo mzuri na wa ushindani tumejiandaa kushindana lolote linaweza kutokea Young Africans ni timu kubwa inawachezaji wengi wazuri lakini tunahofia zaidi mchezaji aliyevaa jezi namba 9 (Mayele) na namba 6 (Fei Toto),”

“Tumekuja kupambana tutapambana hadi dakika ya mwisho bado tuna nafasi ya kufanya kitu  dakika 90 ndio zitaamua nani anatakiwa kuendelea hatua inayofuata,” amesema Kocha Deng

Katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza Feisal Salum ‘Fei Toto’ alifunga bao moja, huku Fiston Mayele akiwaadhibu Mabingwa hao wa Sudan Kusini kwa kutupia mabao matatu pekee yake.

Ikumbukwe kuwa mshindi wa jumla wa mchezo wa kesho kati ya Young Africans dhidi ya Zalan FC atakutana na mshindi wa jumla wa mchezo kati ya Mabingwa wa Ethiopia St George dhidi ya Mabingwa wa Sudan Al Hilal.

Katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Ethiopia St George iliibuka na ushindi wa 1-0, hivyo kujikomboa kwa Al Hilal katika mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa mwishoni mwa juma hili kutategemea na matokeo watakaoyapata wakiwa nyumbani nchini Sudan.

Bungeni: Kuoana ni baada ya miaka sita - Dkt. Stergomena
Watatu Young Africans kuikosa Zalan FC