Katika kuhakikisha inakuwa na kikosi kipana, kikali na chenye uwezo wa kufanya lolote msimu ujao, Everton imeendelea kukiongezea sumu kikosi chake kwa kumnasa beki wa kati kutoka nchini England, Michael Keane kutoka Burnley kwa mkataba wa miaka mitano.

Keane mwenye umri wa miaka 24 amejiunga na Everton kwa ada ya uhamisho ambayo itapanda na kufikia rekodi ya klabu ya Pauni milioni 30 ambayo kwa sasa inashikiliwa na mlinda mlango, Jordan Pickford aliyetua klabuni hapo mwezi uliopita akitokea Sunderland.

Akifanya mahojiano baada ya kukamilisha taratibu zote za uhamisho wake, Keane amesema amejiunga na Everton kwa kuwa ameona ni sehemu sahihi kwake na kuongeza kuwa kocha wa klabu hiyo Mdachi, Ronald Koeman ndiye aliyemvutia hata akakubali kumwaga wino klabuni hapo kwa kuwa na yeye alikuwa akicheza nafasi ya beki wa kati kama yeye.

Keane aliyejiunga na Burnley Januari 2015 akitokea Manchester United kwa ada ya uhamisho Pauni milioni 2 anaamini kuwa karibu na Koeman kutamfanya ajifunze mambo mengi yatakayomfanya awe mwiba mchungu zaidi kwa washambuliaji wasumbufu.

Keane anakuwa mchezaji wa tano kujiunga na Everton katika kipindi cha usajili barani Ulaya.Wengine ni Jordan Pickford, Davy Klaassen, Henry Onyekuru na Sandro Ramirez.

Uamuzi Wa Kikao Cha Kamati Ya Utendaji
Suma JKT kufungua kiwanda cha kusindika minofu