Kwa mara nyingine meneja wa klabu ya Everton Ronald Koeman amezungumzia suala uwezekano wa kutuma ofa ya usajili wa mshambuliaji kutoka nchini Uholanzi na klabu ya Man Utd Memphis Depay.

Koeman aligusia suala la usajili wa mshambuliaji huyo mwanzoni mwa mwezi huu kabla ya kusimama kwa ligi ya nchini England kwa ajili ya kupisha michezo ya kimataifa.

Meneja huyo kutoka nchini Uholanzi amesema kuna uwezekano wa kufanya mpango wa uhamisho wa Depay itakapofika mwezi Januari mwaka 2017, na anaamini kama atafanikiwa kumsajili kutakua na mabadiliko makubwa katika kikosi chake hususan kwenye safu ya ushambuliaji.

“Kama kutakua na nafasi, hatuna budi kufanya mkakati wa kutuma ofa ya usajili wa Depay, tunaamini kwa sasa hana nafasi katika kikosi cha kwanza pale Man Utd,” Alisema Koeman alipozungumza na vyombo vya habari.

“Nilitamani kuwa na Depay tangu nikiwa Southampton, lakini ilishindikana, ila kwa sasa ninaamini mambo yanaweza kukaa vyema kwa sababu anahitaji kucheza mara kwa mara.”

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22, amecheza michezo minne ya ligi kuu ya soka nchini England kwa msimu huu, jambo ambalo halikua la kawaida wakati wa utawala wa Louis Van Gaal.

#HapoKale
Afariki akiombewa kwa ‘nabii’ Arusha, akutwa hana nguo na nyusi