Korea Kaskazini iko tayari kufanya mazungumzo na Marekani pamoja na Korea Kusini kufuatia taharuki iliyopo kati yao, kwa mujibu wa kiongozi wa kijeshi wa Korea Kaskazini mwenye ushawishi, Jenerali Kim Yong-Chol.

Kupitia tamko la ofisi ya Jenerali Kim ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha ujasusi lililotolewa kuhusu mkutano wake na rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in, Jenerali huyo amesema kuwa Korea Kaskazini ambao walituma ujumbe wa viongozi wake katika hafla za ufunguzi wa mashindano ya Olympics nchini humo waliweka wazi kuwa wako tayari kufanya mazungumzo na Marekani bila kuwepo masharti yoyote ya awali.

Alisema viongozi hao walisisitiza kuwa mazungumzo yanayoanza kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini lazima yaende sambamba na mazungumzo ya uhusiano kati yake na Marekani.

Hata hivyo, kufuatia tamko hilo, Marekani imesisitiza kuwa hatua za kusitisha makombora ya nyuklia zinapaswa kuchukuliwa kwanza kabla ya kufikiria kuhusu mazungumzo.

Hayo yamewekwa hadharani muda mfupi baada ya Korea Kaskazini kueleza kuwa vikwazo vipya vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nchi hiyo na washirika wake ni kuleta vitisho vya kivita katika ukanda huo.

Mashindano ya Olympics yanayofanyika Korea Kusini yameonesha mwanga wa kuleta amani kati ya nchi hizo za Peninsula ya Korea.

Dada wa Rais wa Korea Kaskazini, Kim Yo-jong alihudhuria ufunguzi wa mashindano hayo. Pia, Makamu wa Rais wa Marekani, Vice Pence aliwasili kwenye mashindano hayo lakini ilidaiwa viongozi wa Korea Kaskazini walikwepa kukaa naye meza moja.

Binti wa Rais Donald Trump, Ivanka anahudhuria mashindano hayo yanayoelekea kufungwa lakini Marekani imeeleza wazi kuwa hatakutana na kiongozi yeyote wa Korea Kaskazini.

Askofu Bagonza afunguka kuhusu siasa
Wakimbizi waandamana na wengine kuuawa nchini Rwanda