Korea Kaskazini imesema kuwa inaweza kuahirisha mpango wa kiongozi wake, Kim Jong-un kukutana na Rais wa Marekani, Donald Trump kutokana na matamko pamoja na mazoezi ya kijeshi ya pamoja yanayofanywa kati ya Marekani na Korea Kusini.

Kupitia tamko lililotolewa na Makamu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, nchi hiyo imelaani kauli zilizotolea na Mshauri wa Mambo ya Ulinzi wa Marekani, John Bolton dhidi yake.

Aliielezea kauli ya Bolton aliposikika akidai kuwa Korea Kaskazini inaweza kufuata nyayo za Libya katika kuachana na mpango wa silaha zake kuwa ni kutaka kufananisha hatma ya taifa hilo na ile ya Libya iliyokuwa ikiongozwa na Muammar Gaddafi au Iraq ya Saddam Hussein.

“Ni jambo lisilokubalika na hatua mbaya kutaka kuingiza hisia za hatma ya Libya au Iraq, mataifa ambayo yalianguka kutokana na jitihada za kutaka kuharibu nguvu za nchi hizo,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, Korea Kaskazini pia imesema kuwa inashangazwa na kauli za Marekani kuitaka isalimishe silaha zake zote za nyuklia bila masharti yoyote kabla ya kufanyika kwa mkutano huo unaosubiriwa kwa hamu kuweka historia.

Imesema kuwa kwa kauli hizo, Marekani imekuwa inafanya uchokozi hata kabla ya mkutano na kutoa taarifa na matamko ambayo yako kinyume na mpango wanaoendelea nao.

Imefafanua kuwa haitaacha kuweka wazi hisia zake dhidi ya hatua yoyote inayochukuliwa na Marekani wakati ambapo viongozi wa mataifa hayo wanajipanga kukutana nchini Singapore kwa lengo la kurejesha hali ya amani na maelewano katika eneo la Rasi ya Korea.

Katika hatua nyingine, Korea Kaskazini imelaani hatua za majeshi ya Marekani na yale ya Korea Kusini kuendelea kufanya mazoezi ya pamoja, ikidai kuwa mazoezi hayo yanaonesha uchokozi wa mpango wa kutaka kufanya uvamizi.

Hata hivyo, Marekani imeeleza kuwa haitaacha kuendelea kufanya maandalizi ya mkutano kati ya Trump na Kim Jong-un, kwani tuhuma zilizotolewa na taifa hilo bado hazijawasilishwa rasmi kwao. Pia, taarifa ya Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa Kim Jong-un alibariki mazoezi ya kijeshi ya pamoja ya mataifa hayo kwani ni ya kawaida.

Sintofahamu kati ya mataifa hayo yameibuka wakati ambapo Korea Kaskazini imetangaza mpango wake wa kuteketeza maeneo ya majaribio ya silaha za kinyuklia, May 23 hadi 25 mwaka huu, wiki chache kabla ya mkutano wa viongozi wa nchi hizo.

 

Israel, Palestina washambuliana kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa
Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Mei 16, 2018