Shirika la Habari la Serikali ya Korea Kaskazini – KCNA, hii leo Jumatatu Machi 13, 2023 limeripoti kuwa Korea Kaskazini imefanya majaribio ya makombora mawili ya kimkakati yaliyorushwa kutoka kwenye manowari ili kuonesha uwezo wake saa chache kabla ya Marekani na Korea Kusini kufanya luteka kubwa ya kijeshi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, imesema Manowari hiyo ilifyatua makombora hayo siku ya Jumapili Machi 12, 2023 karibu na mji wa Pwani ya Mashariki wa Sinpo na kwamba majaribio hayo yamefanikiwa, kwani yalipiga sehemu zilizokusudiwa ambazo hazikubainishwa katika pwani ya mashariki ya rasi ya Korea.

Urushaji wa Makombora. Picha ya Bannedbook.

Majaribio hayo, ya Korea Kaskazini yanajiri saa chache kabla ya Korea Kusini na Marekani kuanza luteka kubwa zaidi ya kijeshi katika kipindi cha miaka mitano huku Pyongyang ambayo inamiliki silaha za nyuklia imekuwa ikionya kwamba mazoezi kama hayo yanaweza kuchukuliwa kama tangazo la wazi la vita.

Ripoti ya KCNA, imebaini kuwa jaribio hilo linadhihirisha msimamo wa Korea Kaskazini wa kukabiliana na mabeberu wa Marekani na vibaraka wa Korea Kusini, ambapo Wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini imesema Marekani inaanda njama ya kuitisha mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, ili kwenda sambamba na luteka hiyo ya pamoja.

Polisi yawataka Waendesha Baiskeli kutii sheria usalama barabarani
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Machi 13, 2023