Wakati kukiwa na taharuki kati ya Marekani na Korea Kaskazini kuhusu matumizi na majaribio ya mabomu ya nyuklia yanayofanywa na nchi hiyo ya bara la Asia, imetoa msisitizo wa vitisho vingine.

Makamu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, Han Song-ryol ameiambia BBC kuwa nchi hiyo haiogopi vitisho vya Marekani na kwamba wamejipanga kufanya majaribio ya makombora yake kwa mfumo wa kila wiki, kila mwezi na kila mwaka.

Alisisitiza kuwa vita kamili ya nchi hiyo itakuwa ni matokeo ya Marekani kuchukua hatua zozote za kijeshi dhidi yake.

“Kama Marekani inapanga mashambulizi ya kijeshi dhidi yetu, tutajibu kwa makombora ya nyuklia kwa namna yetu na njia yetu wenyewe,” Han anakaririwa na BBC.

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence kuionya Korea Kaskazini kuwa muda wa kuivumilia umekwisha na kuwataka waache kuijaribu Marekani.

Pence alisema kuwa Korea Kaskazini haipaswi kumjaribu Rais Donald Trump akiwataka kuona mfano wa kipigo alichowashushia Syria na Afghanistan hivi karibuni.

Korea Kaskazini imeendelea na mpango wake wa kuandaa na kufanya majaribio ya mabomu ya nyuklia ingawa hatua hizo zimekuwa zikilaaniwa vikali na Umoja wa Mataifa.

Nchi hiyo imelenga katika kuhakikisha inatengeneza makombora yanayoweza kufika katika pande kadhaa za dunia ikiwa ni pamoja na Marekani.

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kuwa mpango huo hautawezekana na tayari ameanza kutuma vikosi vya Marekani na Manuari za kivita katika ufukwe wa Korea.

 

Tanzania Kupeleka Mwamuzi U17 AFCON
Nape: Nikiyakumbuka Haya... Naonekana Mkorofi