Mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo ametoa siku nne kwa vyama vya ushirika vilivyopo mkoani pwani kuhakikisha wanaziondoa Korosho zilizopo katika maghala yao na kuzipeleka katika maghala makuu matatu yaliyo elekezwa na serikali ambayo ni ghala la kibiti, Mkuranga,na Tanita kabla hazijaanza kununuliwa wiki ijayo.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na viongozi wa idara za mkoa na wilaya baada ya kutembelea ghala la kuhufadhi Korosho na kiwanda cha kubangulia zao hilo kilichopo eneo la Tanita, Halmashauri ya Mji wa Kibaha.

Ndikilo amesema Pwani ina vyama vya ushirika zaidi ya 80 na hadi sasa wamehifadhi Korosho hizo katika maghala yao hivyo huu ni wakati mwafaka wa kuhakikisha zinahamishiwa katika maghala makuu ya Serikali ili ununuzi ufanyike mara moja na kuhakikisha wakulima wanapata stahiki yao kama ambavyo Rais Dkt. John Magufuli ameagiza.

Aidha, mkuu huyo wa mkoa wa Pwani amevitaka vyama hivyo kuendesha mchakato wa kukusanya Korosho haraka ili kuhakikisha wakulima wanafaidika kwa kuuza Korosho zao kwa wakati kwakuwa kuchelewesha, kutachelewesha wakulima kulipwa.

Kwa upande wake, Mpimaji wa Korosho kutoka ghala la Tanita, Joseph Malejkano amesema Korosho zinapofika ghalani hapo hatua ya kwanza wanayofanya ni kukata gunia ili kukagua ubora wa Korosho zilizondani.

Fiesta yasitishwa Dar, "Tunaomba radhi kwa masikitiko makubwa"
Video: Majina ya Mengi na Mo yatumika kwa utapeli, Mbowe aenda mahabusu akisema msiogope