Serikali imeagiza korosho zote inazonunua kwa wakulima kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko kuanza kubanguliwa nchini.

Agizo hilo la Serikali limetolewa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 8 Desemba 2018 wakati akizungumza kwenye Mkutano wa wamiliki wa viwanda vya kubangua korosho kwenye ukumbi wa mikutano kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.

Hasunga alisema kuwa Mkakati wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ni kuwanufaisha wakulima nchini hivyo maamuzi ya kununua korosho ni sehemu ya maamuzi mema kwa manufaa ya wakulima wote.

Amesema wakati serikali inaendelea kukamilisha uhakiki wa wakulima wa korosho pamoja na kuendelea na malipo ya wakulima mpaka hivi sasa tayari wakulima 77,380 wamekwishalipwa hivyo hakuna korosho itakayoruhusiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi bila utaratibu maalumu badala yake korosho zote zitabanguliwa nchini.

Hasunga aliongeza kuwa Korosho zitakazoruhusiwa kwenda nje ya nchi ni zile Tani 2000 pekee zilizonunuliwa mnadani na kampuni mbili kwa utaratibu uliokuwa ukitumika awali.

“Hakuna kampuni yoyote wala mfanyabiashara yoyote anayeruhusiwa kusafirisha korosho nje ya nchi baada ya tamko la serikali kutolewa” Amekaririwa Hasunga

Ameongeza kuwa kutokana na uamuzi huo wa serikali imechukua takwimu zote za korosho zilizozalishwa mwaka jana ambazo zilikuwa bado hazijabanguliwa hivyo haitegemei kusikia wafanyabiashara wakisema wana korosho nyingi walizohifadhi badala yake kuwa wazalendo kwa kusema ukweli.

“Tuwe na uwezo wa kubangua ama hakuna lakini korosho zote zitabanguliwa nchini, hivyo wito wangu kwa wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya ubanguaji usiku na mchana” Amesema

Hasunga aliongeza kuwa serikali imeanza mchakato wa kuwafuatilia baadhi ya wafanyabiashara wenye uwezo wa kujenga viwanda kwa kufunga mitambo ndani ya muda mfupi.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Joseph Kakunda (Mb) amesema kuwa serikali imedhamiria kuimarisha uchumi wa viwanda hivyo Serikali haitakubali kuhujumiwa inapoendelea kuboresha uwekezaji, uanzishaji na uendelezaji wa viwanda.

Amesema kuwa Tanzania ni nchi yenye amani na upendo hivyo wafanyabiashara kote Duniani wana wajibu wa kujitokeza na kuanzisha biashara zao pasina kadhia yoyote.

Ameongeza kuwa mawakala wanaotumiwa kuvuruga uchumi wa viwanda na serikali kwa ujumla wake watachukuliwa hatua zinazopaswa kwa mujibu wa sheria.

Mrembo wa Uganda ang’ara Miss World, afuata nyayo za Mtanzania
Mgogoro wa Burundi na Rwanda wazidi kufukuta