Mkazi wa Chato mkoani Geita, Obadia Frank ambaye pia ni wakala wa Bayport amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za kuchapisha taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook kuhusu mazungumzo kati ya Serikali na wawakilishi wa kampuni ya Acacia.

Akisomewa hati ya mashtaka na wakili wa serikali, Leonard Challo, amedai mshtakiwa huyo ametenda kosa hilo Agosti 8 mwaka huu, katika Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Imedaiwa mbele ya Hakimu Mkazi, Wilbard Mashauri, kuwa siku hiyo mshtakiwa alichapisha taarifa kupitia ukurasa wake wa Facebook uliokuwa ukihusiana na mazungumzo kati ya serikali na kampuni ya Acacia.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kusambaza maneno kuwa “Taarifa kutoka kikao cha mazungumzo kati ya Serikali na wawakilishi wa kampuni ya Acacia kuwa wanasheria wa upande wetu wanashindwa kutafsiri baadhi ya vifungu vya sheria hadi kufikia kuomba msaada kwa wanasheria wa Acacia sasa huoni hivi ni vituko mwizi anakusaidia sheria haahaa haha.”

Inadaiwa aliendelea kusambaza maneno kuwa, “mazungumzo bado yanaendelea lakini wanasheria wetu wamebanwa sana ukizingatia wale jamaa wana vielelezo vyote vya mikataba kiukweli tumuombe Mungu maana Serikali ikitaka kuvunja mkataba na Acacia gharama kubwa zitatuusu.”

“Lakini pia kuendeleza uvyama utatugharimu saana, baada ya mh. Rais Magufuli angewashirikisha mawakili wasomi waliokwishaiva wakili Lissu, wakili Kibatara na Fatma Karume kwenye mambo ya umuhimu kama haya yeye kaleta uchama sasa itatugharimu .// Dicteta Magufuli mist go”. Maneno hayo yanadaiwa kusambazwa na mshtakiwa huyo kupitia mtandao huo wa kijamii wa Facebook.

Imedaiwa mshitakiwa ametenda hayo huku akijua kuwa taarifa hizo ni uongo na zilikuwa na nia ya  kuipotosha jamii.

Hata hivyo mshtakiwa huyo anayetetewa na wakili, Peter Kibatala, amekana kutenda kosa hilo na amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti na kesi hiyo itatajwa Oktoba 16 mwaka huu.

Mahakama imemtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao walitakiwa kuweka bondi ya Sh. milioni tano.


Video Magazeti: JPM atema nyongo, Takukuru wafunguka sakata la rushwa Arusha

Daktari wa Argentina aweka wazi hali ya Aguero
Video: JPM atema nyongo, Takukuru wafunguka sakata la rushwa Arusha