Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Saed Kubenea leo amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu na kusomewa shtaka la kutoa lugha chafu dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.

Hata hivyo, Makonda amekana tuhuma hizo na kesi yake imepangwa kusilizwa tena Disemba 29 mwaka huu.

Makonda anamtuhumu Kubenea kumtolea lugha chafu jana walipokutana na kutofautiana katika kiwanda cha nguo cha TZ TOOKU, kufuatia mgogoro uliokuwepo kati ya wafanyakazi na uongozi wa kiwanda hicho. Makonda aliagiza Kubenea akamatwe kwa madai ya kumuita ‘Kibaka’.

Katika hatua nyingine, Chadema wametoa tamko rasmi kulaani kitendo cha Mkuu huyo wa wilaya ya Kinondoni kuamuru mbunge huyo kukamatwa.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya chama hicho, Tumaini Makene, Chadema wameeleza kuwa alichokifanya Paul Makonda ni matumizi mabaya ya madaraka na kwamba ni kinyume cha sheria.

“Tukitambua kuwa mamlaka ya DC kuamuru watu kukamatwa yamefafanuliwa kisheria na kuwekewa mipaka yake ambayo Makonda amedhihirisha kuivuka katika nyakati tofauti sasa, Mkuu huyo wa wilaya hana mamlaka ya kisheria wala ya kisiasa kuhalalisha amri aliyoitoa ya kumkamata mbunge, tena aliyekuwa anatekeleza wajibu wake, tunamtaka DC Makonda amwachie Ndugu Kubenea mara moja huku tukitoa wito kwa mamlaka zilizomteua kumwangalia kwa makini kama bado anazo sifa za kuwa kiongozi wa ngazi hiyo,”inasomeka sehemu ya taarifa hiyo inayolitaka jeshi la polisi kumuachia huru Kubenea.

Azam FC Kufanya Mazoezi Kwa Njia Za Digitali
Mgombea wa CCM apinga Matokeo ya Lema, aeleza ‘figisufigisu’ zilizofanywa