Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea amezungumzia hali ya vyama vya upinzani nchini baada ya siku zaidi 200 kutimia tangu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa atangaze kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Lowassa alijiunga na Chadema Julai 28 mwaka jana baada ya jina lake kukatwa katika orodha ya wanasiasa waliokuwa wanawania nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM, nafasi iliyoenda kwa Dk. John Magufuli.

Lowassa na Maalim Seif 3

Kubenea ameeleza kuwa siku 200 za Lowassa ndani ya upinzani zimezaa matunda makubwa na kwamba wataendelea kumuenzi kwani amesaidia katika kuviunganisha vyama vya upinzani na kuvipa nguvu zaidi kupitia muungano huo.

“Kwakweli Lowassa tunaweza kumuenzi kama shujaa ambaye kupitia yeye vyama vya upinzani vimeimarika zaidi na kusaidia watu waliokuwa wanaamini hawawezi kuondoka ndani ya CCM na kufanya siasa wakaamini na kukihama chama hicho,” alisema Kubenea.

“Kwa siku 200 za Lowassa tunaona ametupatia mafanikio makubwa. Hata kama tumenyang’anywa ushindi bado tuna nguvu kama chama,” aliongeza mbunge huyo.

Alieleza kuwa Lowassa amesaidia vyama vya upinzani kupata wabunge wengi na madiwani ambao baadhi yao walihama CCM. Mbali na hilo, Kubenea ameeleza kuwa Maalim Seif (CUF) amepata kuungwa mkono zaidi katika mgogoro wa Zanzibar kwa sababu ya nguvu ya Lowassa.

Lowassa aliihama CCM na kusababisha mtikisiko mkubwa ndani ya chama hicho tawala ambapo viongozi wengi wa ngazi za juu akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kukihama chama hicho.

Hata hivyo, sio chama tawala pekee kilichopata mtikisiko, Kishindo cha Lowassa kiliitikisa pia Chadema na CUF. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa alitangaza kukiacha chama hicho na kustaafu siasa wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akitangaza kustaafu nafasi yake na kuwa mwanachama wa kawaida.

 

Utashangaa kilichomtokea Mbwa Kichaa aliyemng'ata Polisi
Kingunge avunja ahadi yake kuhusu Magufuli