Mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Saed Kubenea amesema kuwa yeye kutohudhuria kwenye zoezi la uzinduzi wa kitabu cha sera za Chama hicho haimaanishi kuwa anataka kuondoka kwani kuondoka ni maamuzi na anaweza tekeleza muda wowote.

Ameyasema hayo Jijini Dar es salaam ambapo amesema kuwa hapakuwa na ulazima wowote wa kuhudhuria katika uzinduzi wa kitabu cha sera, na alikuwa katika utekelezaji wa majukumu mengine hivyo wanaohoji kutoshiriki kwake ni watu waliopo kwaajili ya kumchafua.

Aidha, Kubenea amesema kuwa ukumbi ulikuwa mdogo na walitakiwa kuthibitisha ushiriki wao, hivyo ukumbi usingeweza kujaza wabunge wote wa CHADEMA na Dar es salaam hayuko yeye peke yake.

“Naweza shiriki uzinduzi saa nne asubuhi na mchana nikahama, kwahiyo nisihukumiwe kwa kutoshiriki kwangu, kwakuwa haikuwa lazima na hakuna uhusiano wowote baina ya sera na kuhama, na sikuwa peke yangu Dar es salaam tuko zaidi ya saba,” amesema Kubenea.

Septemba 25, 2018 Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilizindua kitabu cha sera za chama hicho toleo la mwaka 2018 kikiwa na sera 12 ambazo zimezungumzia namna ambavyo chama hicho kimejipanga kuinua maisha ya mtanzania, suala lililoibua maswali ni kwanini Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea hajaonekana katika eneo la tukio bila kuwa na taarifa kwa Umma.

Hata hivyo, mbali na hilo Kubenea pia amekuwa nyuma katika majukwaa ya CHADEMA ikiwemo kutoonekana ushiriki wake katika kampeni za uchaguzi mdogo wa majimbo ya Ukonga na Monduli, baada ya kudaiwa kuwa miongoni mwa wabunge walioko mbioni kutimkia CCM kutokana na kutokuwa na maelewano na mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe, tuhuma ambazo yeye amekuwa akikanusha na kudai hakuna wa kumuondoa.

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Oktoba 2, 2018
Hospitali ya Bagamoyo taabani kwa madawa