Uamuzi wa rais John Magufuli wa kufuta sherehe za Uhuru zilizokuwa zimepangwa kufanyika Disemba 9 mwaka huu na kuamuru kiasi cha fedha za maandalizi kielekezwa katika kununua vifaa vya huduma ya afya na kupambana na kipindupindu umepokelewa kwa mtazamo chanya na wananchi wengi.

Rais Magufuli ameelekeza kuwa siku ya Disemba 9 mwaka huu itakuwa siku muhimu ya kufanya kazi za usafi nchi nzima kwa lengo la kupambana kipindupindu huku akieleza kuwa itakuwa siku ya ‘Uhuru na Kazi’.

Hata hivyo, kupitia taarifa rasmi ya tangazo hilo iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Gerson Msigwa, umetolewa ufafanuzi kuwa sherehe hizo zimefutwa kwa mwaka huu pekee lakini zitaendelea mwaka ujao (2016) kwa kuzingatia umuhimu wake.

“Ieleweke kuwa sherehe za Uhuru na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu. Hivyo, sherehe hizi zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia mwaka 2016,” ilieleza taarifa hiyo.

 

Waziri Aliyekumbwa Na Ufisadi Wa Kununua Kalamu Moja Sh 200,000 Achukua Hatua
CCM Washinda Tena Ubunge, Waongeza Idadi Mjengoni