Wakati watanzania wakiendelea kusubiri kusikia sera za wagombea mbalimbali wa vyama vya siasa, usalama wa wanasiasa husika umeonekana kuwa tatizo kubwa.

Jana, Mgombea Ubunge wa Shinyanga Mjini kwa tiketi ya Chadema, Patrobas Katambi alivamiwa na watu wasiojulikana akiwa njiani kurudisha fomu zake kwenye ofisi za NEC, ambapo watu hao walizichana fomu hizo na kutokomea kusikojulikana.

Taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Justis Kamgisha zinaeleza kuwa watu hao wasiojulikana walitekeleza tukio hilo majira ya saa mbili asubuhi.

Watu hao waliligonga gari alilokuwa nalo mgombea ubunge huyo akiendeshwa na mdogo wake, baada ya kusimama wakiamini wamepata tatizo la kawaida la barabarani ndipo walipovamiwa na watu hao waliowanyakuwa fomu hizo na kuzichana kisha wakatokomea.

Katika hali inayoonesha kuwa watu hao walilenga kumkamisha mbunge huyo kurejesha fomu kwa muda, hawakumdhuru kwa njia yoyote ile wala hawakuchukua mali au fedha baada ya kuchana fomu hizo.

Hata hivyo, taarifa za awali zilieleza kuwa mgombea huyo alifanikiwa kujaza fomu nyingine na kuziwasilisha kwa muda.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Kamgisha alisema tayari polisi wameanza kuwasaka watu waliofanya tukio hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

“Ingawa fomu zile zilikuwa zimejazwa particulars za mgombea ubunge, lakini bado ni mali ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi,”alisema Kamanda Kamgisha.

Taarifa zilizotolewa baadae zilieleza kuwa fomu zilizochanwa zilikuwa vivuli vya nakala halisi na kwamba mgombea huyo alikuwa ameficha nakala halisi chini ya kiti cha gari. Hivyo, alizipeleka fomu halisi katika ofisi za NEC.

 

Breaking News: Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye Ahamia UKAWA
Wasanii Wakubwa Kuwapigia Debe Wagombea Urais, Wanapatia Au Wanapotea?