Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema kuwa kundi la Hezbollah la Lebanon ni tishio kubwa kwa usalama wa eneo la Mashariki ya Kati, kauli hiyo ameitoa wakati akiwa anajiandaa kufanya ziara Lebanon.

Ameyasema hayo akiwa nchini Israel katika ziara yake ya Mashariki ya Kati yenye lengo la kukazia msimamo wa utawala wa Marekani dhidi ya Iran ambayo inaliunga mkono kundi la Hezbollah la Lebanon, kundi la Hamas la Palestina na waasi wa Houthi wa Yemen.

Katika mkutano wake na Rais wa Israel, Reuven Rivlin mjini Jerusalem, Pompeo ameyaorodhesha makundi hayo kama taasisi ambazo zinasababisha hatari katika utulivu wa Mashariki ya Kati na Israel.

”Umeizungumzia Hamas, Hezbollah na Houthi. Wote hao wanasababisha hatari katika Mashariki ya Kati, wamedhamiria kuiondoa Israel katika uso wa dunia na tuna wajibu wa kuzuia hilo lisitokee, mnapaswa kufahamu kwamba Marekani imejiandaa kufanya hivyo,”amesema Pompeo

Kwa upande wake Israel imefanya mashambulizi ya mara kwa mara ya anga dhidi ya kundi la Hezbollah nchini Syria, ambako kundi hilo la Waislamu wa madhehebu ya Kishia pamoja na majeshi ya Urusi yanamsaidia Rais wa Syria, Bashar al-Assad kupambana na kundi la waasi na makundi ya wapiganaji yenye Waislamu wengi wa madhehebu ya Sunni.

Aidha, Rivlin amesema Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad al-Hariri hawezi kumueleza mtu yeyote kwamba nchi hiyo imejitenga na kundi la Hezbollah. Rivlin amesema iwapo kitu chochote kitatokea kutoka Lebanon kuelekea Israel, basi Lebanon itawajibika. Kundi la Hezbollah lina wawakilishi katika baraza la mawaziri pamoja na bunge la Lebanon.

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 22, 2019
CCM yaja na mpango mkakati ya kukiimarisha chama