Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewataka viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kushughulikia mara moja mapungufu yaliyopo katika shule ya msingi Ubungo King’ongo baada ya mwandishi wa habari kuripoti uwepo wa wanafunzi wanaokaa chini nyakati za masomo.

Magufuli ametoa agizo hilo leo Januari 18, 2021 wakati akizungumza katika uzinduzi majengo ya Shule ya Sekondari ya Wavulana Ihungo iliyopo wilayani Bukoba mkoani Kagera.

“Kuna shule ipo Dar es Salaam, Ubungo (Balango) bado wanafunzi wanakaa chini, madarasa mengine yamebomoka, madawati yamevunjika Mkuu wa Wilaya yupo, Mkuu wa Mkoa yupo, Mkurugenzi yupo na Mbunge wa Ubungo yupo tena yupo hapa na ni Profesa wa elimu, simama wakuone,” amesema Rais Magufuli. 

“Namshukuru mwandishi ameitoa kwenye mitandao, viongozi wakaanza kusema ni masuala ya kisiasa, hayo ndio napenda kuyajua, nazungumza nikiwa Kagera nikienda Dar es Salaam niyakute madarasa yamekamilika na wanafunzi hawakai chini, nitakwenda kuitembelea, kama wananisikia ‘message sent and delivered,” amesisitiza Rais Magufuli.

Ujenzi wa majengo mapya pamoja na ukarabati wa majengo ya shule hiyo yaliyoharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 10.6 na kuongeza uwezo wa shule kupokea wanafunzi wengi zaidi, idadi hiyo imeongezeka kutoka wanafunzi 640 hadi kufikia 1000.

Mbunge Chadema 'aula' Kamati ya Bunge
Ulinzi waimarishwa Marekani