Hatimaye mmiliki wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga amesema kuwa kilele cha Tamasha la Fiesta lililokutana na kisiki cha kuahirishwa wiki kadhaa zilizopita, litafanyika kabla ya mwaka huu kuisha, yaani mwezi huu.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Clouds FM katika kuadhimisha miaka 19 ya kituo hicho, Kusaga amesema kuwa alifanya jitihada za kuhakikisha tamasha linafanyika ikiwa ni pamoja na kuzungumza na viongozi wa Serikali wa ngazi mbalimbali na hatimaye kumfikia Rais John Magufuli.

Kwa mujibu wa Kusaga, mazungumzo hayo yalizaa matunda zaidi na anaamini kuwa changamoto ile imebadilika kuwa neema kwa tamasha hilo na matamasha mengine yanayoibuliwa nchini.

“Mara nyingine matatizo yanaweza kuzaa mema. Kwasababu nilipata nafasi ya kuzungumza mpaka na mheshimiwa Rais kumwambia kuwa labda eneo sio sawa. Kwa sababu matamasha yanaongezeka, kuna Muziki Mnene, Wasafi, Summer Jam nimambiwa inarudi. Kwahiyo kutakuwa na matamasha hadi 10 kwa mwaka na huwezi kuyazuia,” alisema Kusaga.

Mfanyabiashara huyo ameeleza kuwa wamewasilisha wazo la kujenga uwanja wa ndani kwa ajili ya kufanyia matamasha mbalimbali ya kidini, kisiasa na burudani ili kuepuka changamoto iliyojitokeza kupitia Tamasha la Fiesta.

“Imepenyezwa kwa Mkuu wa Mkoa, kwa Meya na hadi kwa Rais… kwamba kuangalia hasa sisi kama Clouds kuweza kupata eneo maalum la kujenga stadium (uwanja wa ndani) ambayo inaweza kubeba hata watu 10,000 hadi 15,000. Unaweza kutumika kwa matamasha, mikutano ya dini zote. Hakuna sehemu hiyo sasa,” alisema na kusisitiza kuwa kwa kushirikiana na wadau wake wanauwezo wa kujenga uwanja huo wa ndani.

Katika hatua nyingine, Kusaga ambaye hakutaja tarehe maalum ya kufanyika kilele cha tamasha hilo mwaka huu, alisema kuwa huwa hawapati faida katika tamasha hilo na kwamba wanafanya kwa lengo la kusogeza muziki mbele.

Alisisitiza kuwa yeye pamoja na wanakamati wote wa tamasha hilo ambao ni zaidi ya watu 15 wanafahamu kuwa hakuna faida ya kifedha wanayoipata kupitia tamasha hilo kubwa tofauti na wengi wanavyodhani.

Mwaka huu, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilizuia kufanyika kwa kilele cha Tamasha la Fiesta katika viwanja vya Leaders na kuelekeza kuwa tamasha hilo lifanyike katika viwanja vya Tanganyika Packers vilivyoko Kawe jijini Dar es Salaam.

Kufuatia maagizo hayo, Kamati ya Fiesta ilitangaza kuahirisha tamasha hilo kwa sababu ambazo walisema ziko nje ya uwezo wao. Leo, Kusaga ameweka wazi kuwa hawawezi kuutumia uwanja wa Tanganyika Packers kwakuwa una changamoto nyingi.

Vichanga 10 wanusurika kukeketwa
Mahakama Kuu yapiga chini marufuku ya Serikali kuhusu daladala

Comments

comments