Kutoka ‘Zenji’

Tangu soka la Zanzibar kuwa na mashakani sasa linafika mwaka mmoja na miezi mitatu bado viongozi wakuu wa chama hicho wanavutana na hii kupelekea kuzidi kuwaumiza wadau wa soka Visiwani Zanzibar.

Ilianza kama masihara mwishoni mwa mwaka 2014 Makamu Urais wa Unguja wa chama kinachosimamia mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) Haji Ameir (Mpakia) kwenda Mahakamani kufungua Kesi nambari 62 ya mwaka 2014 dhidi ya viongozi wenzake wakuu wa ZFA Ravia Idarus Faina (Rais ZFA), Kassim Haji Salum (Katibu ZFA) na Ali Mohammed (Makamo rais ZFA Pemba).

Jambo hilo limepelekea soka la Zanzibar kuathirika sana kwa sekta tofauti ambapo miongoni mwa athari zilizoikumba ni kuchezwa ligi pasipo na udhamini wowote ambapo kila mdhamini ambao awali walionesha nia ya kudhamini ligi hiyo walikimbia upesi wasije kupata aibu kwa ligi ambayo wanaidhamini wao ina mushkeli.

Awali Ligi kuu ya Zanzibar ilikuwa iyanze tangu tarehe 15/9/2015 lakini ilisimamishwa na mahakama kufutia timu ya Chuoni na Aluta kuifungulia kesi ZFA, jambo ambalo lililopelekea mpaka ligi hiyo kucherewa kuanza na ilianza Mwezi Novemba mwaka Jana (2015).

Rundo la timu kupandishwa kiholelea lilijitokeza ambapo msimu ulopita wa mwaka 2014-2015 ligi kuu soka Zanzibar ilikuwa inatimu 12 tu, lakini msimu huu ni vichekesho timu 29 ligi hiyo imejumuisha, timu 15 za Unguja na timu 14 za Pemba ambapo kuna timu zilitoka ligi daraja la pili taifa hadi ligi kuu pasipo hata kupita ligi daraja la kwanza taifa.

Jambo hilo likapelekea ligi kuchezwa viwanja ambavyo havina hadhi ya kuchezwa ligi kuu ya nchi, uwanja wa Bweleo na uwanja wa Wimbi Ndijani, ambapo wadau wengi wa soka wakaanza kuita ligi hiyo majina tofauti, mara Kipwida na wengine waliita Bonanza tu na sio ligi.

Athari nyengine iliojitokeza ligi inachezwa lakini kwa kanda moja tu ya Unguja ambapo ni ligi kuu ya Zanzibar lazima ichezwe kanda zote mbili yani kanda ya Unguja na Pemba, lakini pia kati ya timu 15 za Unguja, tmu 14 zilikubali kucheza ligi isipokuwa timu moja tu ya Malindi kususia kucheza ligi hiyo kwa kutoitambua kamati ya muda iliongoza ligi hiyo.

Soka la Zanzibar kwa kipindi likawa lipo Mahakamani jambo ambalo vilabu vya Zanzibar vilipata hasara kubwa kuhudumia timu zao pasipo hata kuchezwa ligi, na wachezaji walivunda maana walifanya mazoezi kusubiri ligi mpaka wengine walishindwa na kupelekea hata vifaa vyao vya michezo kufanyia shughuli nyengine.

Tarehe 2/9/2015 Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) ilisimamisha kozi zao zote kufanyika Zanzibar zikiwemo hata kozi za Makocha ambapo ilikuwa tayari ishaandaliwa Kozi ya makocha ya leseni B iliokuwa ifanyike kuanzia tarehe 5/9/2015 ambapo CAF iliitumia barua ZFA kuwa kozi hiyo wameizuia kutokana na soka la Zanzibar kuwepo Mahakamani.

ZFA iliathirika sana mana Mkufunzi wa kuendesha kozi hiyo Sunday Kayun alikuwa tayari kashakatiwa tiketi ya Ndege kwa ajili ya kuja kuwanowa makocha Visiwani na
Makocha wengi walipata hasara kwa hilo maana walikuwa wanatarajiwa kushiriki katika kozi hiyo ni makocha wa Zanzibar, Tanzania bara na mmoja kutoka Zambia, ambao ni Ibrahimm Mohd Makeresa, Omar Khamis Othman, Abubakar Issa Simai, Ali Suleiman Haji, Mohd Abass Silima, Ramadhan Abdulrahman, Yussuf Ramadhan, Sheha Khamis Rashid, Salim Haji Mwadini, Iddi Mohd Ali, Ali Abdallah Hassan, Juma Awadh Khatib, Juma Yussuf Sumbu, Mzee Ali Abdallah, Hafidh Muhidin Mcha, Mussa Hassan Jaribu, Asaa Khamis Mtwana, Hamad Mzee Shilingi, Jumanne Chalse, Mbwana Mtem, Renatus Shija, Tegete, Mrage Kabange, Ali Mohd Ameir, Seif Bausi, Bakar Ali Hamad, Saleh Alawi Abdallah, Suleiman Mahmoud, Masoud Salum Abdi na wa mwisho ni David Solopi ni kutoka Zambia.

Jumla ya makocha wote hao wamekosa fursa ya kozi hiyo, pengine wakizidi kusaidia soka la Zanzibar baada ya kupatiwa mafunzo hayo.

Hilo ni soka la Zanzibar ambalo limechafua kila sehemu kwasasa, wawakilishi wa Zanzibar katika michuano ya Kimataifa ya klabu bingwa na kombe la shirikisho timu ya Mafunzo na JKU nao waliathirika na hilo la Soka kuwepo Mahakamani maana hata maandalizi yao yalikuwa ni ya kusuwa suwa, mara wanaambiwa hamtoshiriki, mara mtashiriki, hili pia limewatoa mchezoni wachezaji wa timu hizo japo kuwa JKU amesonga hatua nyengine ya kombe la Shirikisho kufuatia wapinzani wao timu ya Gabarone United ya Bostwana kujitoa katika mashindano hayo.

Hii inaonesha hata Mafunzo ambae ni bingwa mtetezi wa ligi kuu soka Zanzibar angeweza kufanya vizuri au hata kupunguza idadi ya mabao katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika alipotolewa na AS Vita Club ya DR Congo ambapo jumla kafungwa mabao 4-0 kufuatia 0-3 alizofungwa nyumbani kwao Zanzibar na 1-0 alilifungwa huko DR Congo jumapili ilopita.

Jumamosi ya tarehe 27/2/2016 ZFA walifanya Mkutano mkuu wa dharura wa ZFA TAIFA ambapo wajumbe waliamua maamuzi mazito katika mkutano huo.

Ajenda tatu zilijadiliwa katika mkutano huo ambao ulifanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Kikwajuni Mjini Unguja ambapo miongoni mwa mada tatu zilizojadiliwa, moja ni kujadili mwenendo wa kamati tendaji ambapo muwasilishaji wa mada hiyo alikuwa Makamu wa Urais ZFA Unguja Haji Ameir (Mpakia) ambae hakuonekanwa katika mkutano huo na mada yake hiyo ikawasilishwa na Makamu wa Urais ZFA Pemba Ali Mohammed.

Baada ya kusikiliza mada hiyo wajumbe 50 waliokuwepo kwenye ukumbi huo wamekubaliana kupiga kura, kura ambayo ilikuwa inamuhusu Makamu wa Urais Unguja Haji Ameir aliepeleka kesi ya soka Mahakamani mwishoni mwa mwaka 2014 ambapo wajumbe walitaka afukuzwe kwenye chama hicho na asijihusishe na mambo ya michezo kwa muda wa miaka 4.

Wajumbe 50 wakapiga kura ambapo wajumbe 43 walisema afukuzwe na wajumbe 4 walisema asifukuzwe ambapo wajumbe 3 hawajapiga kura.

Hivyo, Alhaj Haji Ameir ambae ni Makamu wa Urais ZFA Unguja alifutwa rasmi nafasi hiyo na kutojishughulisha na mambo ya michezo kwa muda wa miaka 4.

Aidha mkutano huo uliiyondoa kamati ya muda iliokuwa ikiongoza soka la Zanzibar ambapo wajumbe 42 walisema kuwa kamati hiyo iondoke na wajumbe 6 walisema wasiondoke wakati wajumbe 2 kati ya hao 50 hawajapiga kura.

Ajenda ya pili iliyowasilishwa katika mkutano huo kuhusu kuteuliwa Mkaguzi wa Mahesabu yaani ‘Auditors’ kwa ajili ya kuvipitia vitabu vya mahesabu vya Chama hicho ambapo mkutano huo umekubaliana kuchaguwa Kampuni yenye sifa kufanya ukaguzi wa Mahesabu kwa ZFA Taifa ambapo utafanyiwa tangu uongozi wa ZFA wa mwaka 2012 hadi 2016, yani kipindi cha Rais Amani Makungu na Ravia Idarous Faina wa sasa.

Na ajenda ya tatu mkutano mkuu ulikuwa unatakiwa kuamua kuteuwa wajumbe 5 watakaoandika upya Katiba ya ZFA ambapo wajumbe 5 walioteuliwa kati ya hao 12 waliopendekezwa Awali ni Eliud Peter Mvella kura 46 (Msaidizi mkurugenzi TFF na Mwanasheria), Saleh A. Said kura 43 (Wakili upande wa ZFA), Affan Othman Juma kura 42 (Kiongozi wa mpira na taaluma ya sheria) Ame Abdalla Dunia kura 40 (Mwalimu/Taaluma ya Sheria), na Othman Ali Hamad kura 36 (Mwanasheria, Kiongozi na mchezaji wa mpira).

Aidha mkutano huo umehalalisha wajumbe waliokuwepo kwenye ZFA Wilaya ya Magharibi “B” kuwa ni halali na wanatambuliwa na mkutano mkuu na hautofanyika tena uchaguzi kwenye Wilaya hiyo.

Kuhusu uchaguzi wa ZFA Taifa mkutano huo umetowa tarehe ya kufanyika Uchaguzi huo ambao unatarajiwa kufanyika April 9, 2016 huko Kisiwani Pemba ambapo nafasi ya Urais, Makamu Urais Pemba na Makamu Urais Unguja ndizo nafasi tatu zitagombaniwa katika uchaguzi huo ambapo pia katiba itakayotumika ni ya mwaka 2010.

Jambo jengine katika mkutano huo ni Ligi kuu soka Zanzibar kanda ya Unguja ambayo imeendeshwa na Kamati ya Mpito iliofutwa leo hii, kwa makubaliano ya mkutano huo ligi hiyo wamesema ni halali na wanaikubali, na ligi kanda ya Pemba karibuni itaanza kuchezwa baada ya kukaa kamati tendaji.

Lakini baada ya kufutwa Makamu Urais ZFA Unguja Haji Ameir (Mpakia) yeye alisema kuwa ni ukiukwaji wa katiba na sheria walichofanya wenzake kumuondosha katika chama hicho na kusema kuwa hawana uwezo wa kumfukuza na yeye atarudi tena Mahakamani.

Soka la Zanzibar linazidi kusikitisha kitu si kitu Mahakamani na hili wadau wengi wa soka ambao hawajapenda majina yao kuandikwa humu walisema kuwa viongozi wote wanaongoza ZFA hawafai na waondoshwe wote ili soka linusurike.

“ ZFA nzima haifai na wao ndio wanatuharibia mpira wetu, ili soka letu lirudi hadhi yake kama ya zamani, basi viongozi wote wa ZFA hawafai waondoke, wanatuumiza , hatuwataki, kila siku Mahakamani ndo nini!, Mpakia, Ravia na Ali Mohammed wote hawafai, wajiuzulu tumewachoka, sisi tunajua pale ZFA pana rundo la pesa ndo mana hawataki kuondoka, na sijui kama hawatorogana, hatuwataki watuachie mpira wetu kwasababu tunaongozwa na watu ambao si wa Mpira”. Walisema Wadau.

Hilo ndio soka la Zanzibar bado halijakaa sawa sawa mpaka leo tangu mwaka 2014 lilipokwenda Mahakamani ambapo kwasasa kesi hizo zimeshafutwa.

Samia Suluhu asema mgogoro wa Zanzibar umesababishwa na 'wana CCM, mamluki'
Zanzibar Judo Warejea Visiwani Na heshima ya ushindi