Kwa mara nyingine jana makontena 20 ya Paul Makonda yalikosa mnunuzi bandarini, licha ya matumaini ya awali ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa kulikuwa na dalili nzuri zaidi kuliko wiki iliyopita, huku idadi ikizua jambo.

Baadhi ya watu waliokuwa wanashiriki katika mnada huo walieleza kuwa kuonekana kwa makontena 10 pekee katika siku ya mnada badala ya makontena yote 20 ni moja kati ya vitu vilivyozua wasiwasi.

Akijibu kuhusu kutoonekana kwa makontena mengine 10 kwenye mnada huo ulioanza majira ya saa tatu asubuhi, afisa mwandamizi wa TRA ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema hilo pamoja na mambo mengine lilitokana na ufinyu wa nafasi ya eneo la mnada.

“Tulifikiria pia ukweli kuwa washiriki wote wa mnada walipewa siku tatu kuyaangalia makontena yote 20 na bidhaa zilizomo, hivyo hatukuona haja ya kuyabeba tena yote 20,” The Citizen inamkariri.

Aidha, suala la bei lililalamikiwa pia na baadhi ya washiriki wa mnada huo uliokuwa ukifanywa na kampuni ya Yono Auction Mart.

“Hata kama wewe ndiye ungekuwa mnunuzi, ungeweza kununua haya kwa Sh20 milioni wakati thamani yake ni Sh10 milioni. Sio sawa. Halafu, makontena yenyewe [ndani] hayajapangwa vizuri,” alisema Ibrahim Jongo aliyeshiriki mnada huo.

Aliongeza kuwa wakati anaangalia makontena hayo, hakuona makontena yenye viti na masofa au meza.

Wakati wa mnada huo, Mkurugenzi Mkuu wa Yono Auction Mart, Sholastica Kevela aliwatahadharisha waandishi wa habari kutopiga picha za bidhaa yoyote iliyo ndani ya Makontena.

Kiasi cha juu zaidi kilichotajwa na washiriki ni takribani Sh16 milioni, lakini hakikufikia kiwango cha chini kilichokusudiwa. Hata hivyo, Yono Auction Mart hawakuweka wazi kiwango cha chini zaidi kinachotakiwa wakisema kuwa TRA ndio wenye mamlaka hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewahi kueleza tangu Mei mwaka huu kuwa makontena hayo yana samani kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ufundishaji ya walimu wa mkoa huo na kwamba ni msaada kutoka kwa rafiki zake wa Marekanji.

Waziri wa Fedha, Philip Mpango aliagiza makontena hayo yapigwe mnada hadi yapate mteja, baada ya Makonda kushindwa kulipia kodi.

Mwanafunzi aliyeuawa kwa kichapo azikwa
Kalanga amrudia Lowassa kivingine, ‘nimeongea na wazee’