Naibu Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ushetu, Elias Kwandikwa amefanya ziara ya kikazi katika Kata ya Igwamanoni ikiwa na lengo la kukagua changamoto mbalimbali za elimu zinazilikabili jimbo hilo.

Katika ziara hiyo, Mbunge alipata fursa ya kukagua shule ya Sekondari Igwamanoni, shule ya msingi Luhaga na Shule ya msingi Iramba ambapo alibaini upungufu wa madarasa ya Shule ya Sekondari Igwamanoni hali iliyomlazimu kutoa pesa kiasi cha Tsh 1,500,000/= ili kusaidia umaliziaji wa jengo la vyumba viwili vya madarasa na kiasi cha Tsh 500,000/= kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa shimo la choo cha wanafunzi Shule ya Msingi Iramba.

Kwandikwa amekabidhi Tsh 500,000/= kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa choo cha shule ya msingi Luhaga pia amefanya mikutano ya hadhara na wananchi katika vijiji vya Luhaga, Igwamanoni na Iramba akiwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kutatua changamoto zinazowakabili hasa kuboresha huduma za jamii ikiwemo maji ambayo tayari kisima kirefu kimeshachimbwa katika Kijiji cha Iramba huku kazi Iliyobaki ni usambazaji kwa Wananchi.

Aidha, kuhusu sekta ya miundombinu ya barabara, amesema kuwa Barabara ya Mpunze, Luhaga, Iramba na Idahina zimeshapata Mkandarasi ambaye tayari yupo eneo husika kwa utekelezaji wa Ujenzi wa Barabara hiyo huku akiwajulisha wananchi wa kitongoji cha Bufuko kuwa barabara inayowaunganisha na Kijiji chao cha Luhaga yenye urefu wa Km 5 itatengenezwa katika kipindi hiki na kuongeza kuwa vijiji 6 vya kata ya Igwamanoni vitapatiwa umeme wa REA awamu ya tatu.

Kwaupande wake Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Kahama, Johakimu Simbila amesema kuwa chama cha Mapinduzi wilayani humo kimeendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Elias Kwandikwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu, Juma Kimisha na Mkurugenzi wa Ushetu, Matomola ambao kwa pamoja wanaendelea kushirikiana kutafuta namna ya kukabiliana na umaliziaji wa majengo ya Zahanati, Madarasa na Nyumba za watumishi zilizojengwa kwa nguvu za wananchi.

Kangi Lugola ateta na UNHCR kuhusu wakimbizi
Aweso atumbua mkandarasi wa maji mkoani Kagera

Comments

comments