Tatizo la ajira linawatesa vijana wengi wenye elimu nchini, vijana wengi wamekuwa wakiitwa kwenye usaili mara kwa mara na kufika hata hatua ya usaili wa maneno (oral interview), lakini ndoto zao za kupata ajira huishia mlangoni.

Wengi wamekuwa wakitumia muda mwingi kujifua kwa jinsi watakavyojibu maswali yatakayoulizwa katika usaili, juhudi ambazo huonekana zimezaa matunda wakati wa usaili kwani hujikuta wakipata majibu sahihi ya maswali mengi yanayoulizwa na wasaili. Lakini mwisho hujikuta wakishindwa kuitwa kazini na nafasi zao kuchukuliwa na watu wengine. Hali hii huwafanya wengi kukata tamaa na kuhisi kuwa hakuna kazi bila kujuana au kutoa rushwa, bila kufanya tathmini zaidi ya kile walichokisema kwenye usaili huo.

Sababu za kushindwa usaili ingawa umejibu vizuri maswali:

Nje ya chumba cha usaili

Usaili wa kazi hauanzii pale unapokuwa unazungumza na wasaili pekee. Pia, unapaswa kufahamu kuwa alama za usaili hazihusishi majibu yako pekee au muonekano wako wa utanashati mbele ya wasaili husika.

Ukweli ni kwamba, katika maeneo mengi hususan kazi ambazo zina unyeti au ushindani mkubwa, usaili huanzia katika muda wa kuwasili katika usaili huo na kila utakachofanya wakati ukiwa katika mazingira ya usaili huo kinaweza kuhesabika pia kama sehemu ya usaili.

Interview 4

Unashauriwa kufika nusu saa kabla ya muda wa kuanza usaili huo na sehemu utakayoelekezwa kukaa na kusubiria usaili, ichukulie kama sehemu ya chumba cha usaili wa awali, hivyo, mkao wako na jinsi unavyoonekana muda wote lazima uendane na mtu anaehitajika. Onesha kujiheshimu na kujiamini muda wote unapokuwa pale. Simu yako inaweza kukupunguzia umakini wa usaili, hivyo ni bora uiache.

Wasalimu kwa heshima na kujiamini watu wanaopita katika maeneo hayo kwani wanaweza kuwa wasaili au watu wanaoweza kufanya mapendekezo katika nyanja za tabia nyinginezo.

Ndani ya Chumba cha usaili

Unapokuwa ndani ya chumba cha usaili, mbali na maswali unayoyajibu kwa ufasaha, tabia nyingine za kwako zinaweza kuonekana kupitia lugha ya mwili wako kila sekunde unayokuwa katika usaili huo.

Matt Eventoff, mtaalam wa masuala ya mawasiliano ya umma wa Marekani anaeleza kuwa kila mtu ana lugha ya mwili ambayo amekuwa nayo kutokana na mazoea. Na lugha hizo za mwili zinaweza kuzungumza kwa sauti kubwa zaidi ya sauti yako wakati unajieleza.

Unapokuwa kwenye usaili, lugha ya mwili huzungumza zaidi wakati unaongea na pia huhesabika, hii ndio sababu alama mojawapo kubwa katika usaili ni ‘kujiamini’.

Interview 6

Wapo watu wengi ambao wamezoea kufanya ishara fulani za mwili bila kuelewa, wapo watu ambao hawawezi kupitisha dakika moja bila kugusa ‘pua’ kwa mfano. Wapo ambao huvunja vidole wakati wanazungumza, wapo ambao kila wanapotafakari jambo hujishika kidevuni au kichwani. Hizi zote ni sehemu ya lugha kubwa za mwili na zinatoa maelezo zaidi. Kwa mfano, wataalam wa saikolojia wanasema kuwa mtu anaposema uongo, macho yake hutofautiana na anachokieleza. Kugusa pua pia inahusishwa na hilo.

Kuvunja vidole, kuvuta kikohozi, kuchezea ncha za nywele kwa wasichana pamoja na kicheko kikavu ni sehemu ya ishara ya kutojiamini na kutokuwa na uhakika na unachokisema au kusema uongo.

Epuka kukwepesha macho yako unapojibu maswali au unapoulizwa maswali, kama wasaili wapo zaidi ya mmoja, muangalie usoni kila anaekuuliza swali na uoneshe kuwa makini kumsikiliza, fanya hivyo pia unapomjibu. Hakikisha unapunguza kadiri iwezekanavyo lugha za ishara kwa kuwa zinaweza kuongea zaidi ya kile unachoelezea na kukupunguzia alama. Hata hivyo, hutakiwi kukaa kama ‘robot’ au sanamu ili usitoe ishara.

Interview 3

Usiweke mikono mfukoni au kuikunja kifuani wakati unaongea. Onekana kama mtu ambaye yuko wazi kufikiwa na sio mtu mwenye tabia za kutaka kuwa ‘boss’. Weka mikono yako mbele. Unaweza kuona haina maana sana, lakini kuweka mikono mbele ni ishara nzuri ya kuonesha kuwa uko ‘approachable’.

Unashauriwa kuonesha sura yenye furaha hata kama swali lililoulizwa limekuwa zito kwako au limekushinda, hata kama wasaili waonesha huzuni au wanaonesha usoni kuwa hawaridhiki na unachokisema. Usipaniki, usitumie ishara nyingi kutaka kuwaelewesha bali waoneshe sura ya ukarimu kwani kila mwajiri anamuona mtu anaetaka kumuajiri kama sura ya kampuni au ofisi yake.

Pia, kuna wakati wasaili wanaweza kukuwekea presha kubwa hasa pale wanapoona unajua vitu vingi, hivyo wakataka kukupa changamoto za presha waone utafanya nini. Kama kuna muda unaopaswa kutulia na kuweka kando tabia zako za kupambana kwa nguvu kubwa na hoja ni huu. Ni vyema kuonesha kupokea changamoto hizo kwa mtazamo chanya na kwa sura ya furaha, kisha toa shukurani kwa swali au changamoto waliyokuwekea na toa majibu kwa utulivu muda wote.

Gerd Müller Bomber Asumbuliwa Na Alzheimer
Ukaguzi Wa PPRA: NEC Miongoni Mwa Taasisi 9 Kupelekwa Takukuru Kwa Harufu Ya Rushwa