Beki mpya wa klabu ya Arsenal Shkodran Mustafi, amezusha hofu miongoni mwa mashabiki wa klabu hiyo pamoja na wale wa timu ya taifa lake la Ujerumani baada ya kuumia katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki.

Beki huyo amepatwa na majeraha ya kifunzo cha mguu, ikiwa ni saa 24 baada ya kukamilisha usajili wa kujiunga na The Gunners akitokea Valencia CF ya nchini Hispania kwa ada ya Pauni Milioni 35.

Gazeti la The Sun limeripoti kuwa, Mustafi alimaliza mchezo huo uliokua na lengo la kumuaga kiungo Bastian Schweinsteiger aliyetangaza kustaafu mwezi uliopita, akiwa anachechemea kufuatia maumivu makali aliyokua anayahisi mguuni mwake.

Hata hivyo bado haijaelezwa kwa kina kama Mustafi ameumia kwa kiasi kikubwa hadi kufikia hatua ya kutiliwa mashaka ya kuukosa mchezo wa mwishoni mwa juma hili, ambapo Ujerumani wataanza kampeni ya kutetea ubingwa wa dunia kwa kupambana na Norway, katika hatua ya mchujo.

Kama itabainika Mustafi amemua na hatoweza kucheza kwa majuma kadhaa yajayo, itakua ni kama gundu kwa meneja wa Arsenal Arsene Wenger katika kipindi hiki cha mwanzoni mwa msimu.

Tayari mzee huyo ameshamkosa beki na nahodha wake Per Mertesacker katika michezo ya kabla na baada ya kuanza kwa msimu wa 2016/17, kufuatia majeraha ya goti yanayomkabili.

Mustafi anatarajiwa kucheza sambamba na Laurent Koscielny katika michezo ijayo ya ligi kuu ya soka nchini England pamoja na ile ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, lakini taarifa za kuumia kwake zinaendelea kuleta mashaka.

Mbwana Samatta: Nitawasiliana Na Daktari Wa Taifa Stars
Kama Mambo Yangekwenda Vizuri, Sturridge Angetua Emirates Stadium