Beki wa pembeni wa klabu bingwa nchini England Manchester City Kyle Walker amesema angelikua mpuuzi endapo angeliendelea kuwa mapumzikoni katika kipindi hiki, ambacho ni muhimu kwa klabu hiyo kuelekea msimu mpya wa ligi.

Walker amesema alilazimika kusitisha mapumziko yake, baada ya kuitumikia timu ya taifa ya England kwenye fainali za kombe la dunia nchini Urusi, kwa lengo la kuisaidia Man city kwenye mchezo wa ngao wa jamii dhidi ya Chelsea uliochezwa juzi Jumapili jijini London.

Beki huyo alijumuika na beki mwenzake kutoka England John Stones na kusaidia mafanikio ya ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Chelsea katika mchezo huo uliounguruma Wimbley Stadium.

“Kama ningeshindwa kujiungana kikosi kwa kusingizia likizo ya mapumziko ningekua mpuuzi, sikuona umuhimu wa kufanya hivyo kwa sababu, niliamini nina uwezo wa kurejea kujiunga na timu, na nimefanikiwa,” Walker aliwaambia waandishi wa habari.

“Likizo ina muda wake ninaamini utafika wakati nitapumzika lakini linapokuja suala la kuitafutia mafanikio klabu, nipo tayari kufanya hivyo wakati wowote.”

Walker na Stones walipaswa kurejea katika mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzao wa Man City kuanzia jana Jumatatu, kutokana na kumaliza jukumu la kuwa katika timu ya taifa ya England mnamo Julai 14 kwa kucheza mchezo wa mshindi wa tatu dhidi ya Ubelgiji, lakini hatua hiyo imekua tofauti.

Wawili hao bado wanategemewa kuwa sehemu ya kikosi cha Man City katika mchezo wa kwanza wa ligi ya England msimu wa 2018/19, ambao utawakutanisha na washika bunduku wa Ashburton Grove (Arsenal), mwishoni mwa juma hili, jijini London.

Trump kumpokea Kenyatta ‘White House’, aweka historia
Video: Nape, Bashe hawawezi kufukuzwa uanachama- Ridhiwani Kikwete

Comments

comments