Kocha mkuu wa Al Merrikh, Lee Clark ametamba kuibuka na ushindi mbele ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, kwenye mchezo wa kesho wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, hatua ya Makundi.

Clark ambaye ana siku kadhaa tangu alipoanza kazi kwenye klabu hiyo ya mjini Khartoum, Sudan ametoa tambo hizo leo mchana alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es salaam.

Kocha huyo amesema amekiandaa vyema kikosi chake kuelekea mchezo wa kesho ambao utaanza mishale ya saa kumi jioni, Uwanja wa Benjamin Mpaka, jijini Dar es salaam.

Amesema anaiheshimu sana Simba SC kutokana na kuwa na matokeo mazuri katika michezo ya Kundi A, hivyo amejiandaa kukabiliana nayo kwa heshima lakini atahakikisha mwisho wa mchezo anakuwa na kicheko cha furaha.

“Nawashukuru kwa kuwa hapa, tumejianda tangu tumefika, wachezaji wapo vizuri tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Simba. Tunahitaji kupata matokeo chanya ili kufufua matumaini ya kubaki kwenye michuano hii,” amesema Clark.

Naye nahodha wa kikosi cha Al Merrih Ahmed Adam amezungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake kuwa wamekuja Tanzania kuchukua alama tatu muhimu mbele ya Simba na watahakikisha wamefanya hivyo.

“Tulicheza vizuri Sudan lakini hatukupata alama tatu tulizokuwa tumezilenga, hii ya kesho ni mechi muhimu ugenini na tumefika kutafuta ushindi pia kuonesha dunia kiwango chetu hivyo tunatarajia kupata matokeo chanya kwenye mchezo wa kesho,” amesema Adam.

Simba SC itakua mwenyeji kwenye mchezo huo wa mzunguuko wanne wa hatua ya makundi kesho Jumanne (Machi 16), huku ikiongoza msimamo wa kundi A, kwa kuwa na alama saba, ikifuatiwa na AS Vita Club na Al Ahly wenye alama nne kila mmoja, huku Al Merrikh wakiburuza mkia kwa kupata alama moja.

Lwanga kuikabli Al Merrikh kesho
Mabadiliko Young Africans safi