Meneja wa muda wa mabingwa wa soka nchini England, Leicester City, Craig Shakespeare, amesisitiza kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kikosi chake kinarejea kwenye michuano ya barani Ulaya msimu ujao.

Shakespeare alitangaza msisitizo huo dakika chache baada ya mchezo wa mkondo wa pili wa robo fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Atletico Madrid kumalizika kwenye uwanja wa King Power mjini Leicester.

Sare ya bao moja kwa moja imewatupa nje mabingwa hao wa England, ambao walishiriki kwa mara ya kwanza michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya na kufika hatua ya robo fainali.

Ushindi wa jumla wa mabao mawili kwa moja umeipa nafasi Atletico Madrid kutinga hatua ya nusu fainali.

Shakespeare aliwaambia waandishi wa habari kuwa, wana nafasi nyingine wa kucheza michuano ya Europa League msimu ujao, endapo watafanikiwa kupambana katika michezo ya ligi ya England iliyosalia .

“Ninaamini kuna faida kubwa tumeipata kupitia michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, ambayo tumeshiriki kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hii, tutahakikisha tunapambana hadi mwishoni mwa msimu huu, ili tuwe sehemu ya timu zitakazoingia kwenye Europa League msimu ujao,” alisema Shakespeare.

“Tunastahili kujipongeza kwa hatua kubwa tulioipiga kwenye michuano hii, kutokana na juhudu zilizoonyeshwa na wachezaji pamoja na viongozi, tunajua uzuri wa michuano ya Ulaya na hatuna budi kujipanga upya.”

Leicester City hawana nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao, kutokana na nafasi waliopo kwenye msimamo wa ligi ya England kwa sasa, na hata ikitokea wanashinda michezo yao yote iliyosalia, bado nafasi hiyo itakua ndoto kwao.

England ina nafasi nne za ushiriki wa ligi ya mabingwa barani Ulaya na nafasi tatu za ushiriki wa Europa League.

Leicester City kwa sasa wapo kwenye nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi ya England, na kama watafanikiwa kushinda michezo yao sita iliyosalia watakua na uwezo wa kuingia kwenye ukanda wa ushiriki wa Europa League msimu ujao.

Serikali kuzifanyia ukarabati nyumba za NHC
Jamal Kisongo: Mbwana Samatta Ataondoka Ubelgiji