Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amewataka mawakili wake kutofanya lolote bali wamuache aendelee kusota rumande hadi pale upande wa Serikali utakapokamilisha taratibu zake.

Lema alitoa uamuzi huo jana, muda mfupi baada Mahakama Kuu kufuta rufaa ya maombi ya dhamana yake ikieleza kuwa alifikia uamuzi huo kwakuwa maombi hayo yaliwasilishwa nje ya muda unaokubalika kisheria.

“Msiogope, jitieni moyo, nimewaambia msijihusishe na chochote hadi pale upande wa Jamhuri utakapomaliza kazi yake,” Lema anakaririwa kabla ya kupanda kwenye gari kurudishwa rumande ya Gereza Kuu la Kisongo.

Naye mke wa Mbunge huyo, Neema Lema pamoja na baba mzazi wa mbunge huyo walieleza kuwa wamezungumza naye na wamekubaliana kuwa waache kuendelea kukata rufaa kwani kila wakijaribu vinatokea vizingiti.

“Kama familia na nilipoongea na mume wangu Lema tumeona aachwe huyo mtu yafuatwe maagizo yake na afanye atakalo,” alisema Neema.

Hata hivyo, wakili wa Lema, John Mallya alisema kuwa ingawa Lema amewaambia waache kufuatilia, wao wanaona bado kuna namna ya kufanya hivyo watakutana kama jopo na kujadili njia ya kuishawishi zaidi mahakama kupata dhama yake.

Lema anakabiliwa na kesi ya uchochezi ikiwa ni pamoja na kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Rais John Magufuli.

Ni nani msanii wa hip hop namba 1 Tanzania? Nikki wa Pili afunguka
Muhongo: TPDC toeni leseni kwa wakati