Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) na Mkewe Neema Lema, jana walijikuta mikononi mwa polisi kwa nyakati tofauti wakikabiliwa na tuhuma za kutoa lugha ya kuuudhi na uchochezi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema kuwa Lema alikamatwa na kuhojiwa jana na jeshi hilo kutokana na kauli zake dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizotoa katika mkutano wake wa hadhara.

Kamanda Mkumbo aliwaambia waandishi wa habari kuwa lema alitamka, ”Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiendelea kugandamiza demokrasia, siasa za ugandamizaji, Taifa litaingia katika umwagaji damu, nchi hii inaandaliwa kwenda katika utawala wa kidikteta.”

Mbunge huyo pia alikiri kuhojiwa na jeshi la polisi na kudai kuwa anachosubiri ni kupelekwa mahakamani kwani alitoa kauli hiyo kwa nia njema.

Katika hatua nyingine, Mke wa Lema jana aliunganishwa katika kesi ya inayomkabili mumewe ya kumtumia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ujumbe unaotajwa kuwa na lugha za kuudhi.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Blandina Msawa alieleza mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Agostine Rwezile kuwa Neema ameunganishwa katika kesi ya mumewe kwakuwa simu yake ndiyo iliyotumika kutuma ujumbe huo.

Lema alipandishwa kizimbani Agosti 29 mwaka huu akidaiwa kumtumia ujumbe Gambo unaosomeka, ”Karibu Arusha, tutakushughulikia kama mashoga wanavyoshughulikiwa uarabuni.”

Neema aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yote. Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 15 mwaka huu.

Arsenal, PSG, Bayern Munich Zatangulia 16 Bora Ulaya
Chadema yashinda Umeya Manispaa ya Ubungo