Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) ameeleza kutoshangazwa na taarifa za aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kuingia Bungeni na kujibu swali akiwa amelewa kwani awali kulikuwa na bar ndani ya uzio wa Bunge.

Lema ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, aliyasema hayo katika kipindi cha Dakika 45 cha ITV, ambapo alieleza kuwepo kwa tatizo kubwa la ulevi ndani ya Bunge ambalo kimsingi linatokana na kukosekana kwa maadili.

“Wakati wa mikutano ya Bunge la Katiba, kulikuwa na bar mbili ndani ya uzio wa Bunge. Kwahiyo, sishangai suala la mbunge kuingia ndani ya Bunge akiwa amelewa kama mwanzo kulikuwa na mazingira hayo,” alisema Lema na kuongeza kuwa hivi sasa hazioni tena bar hizo katika eneo la Bunge.

Alisema kuwa tatizo la ulevi linalitafuna Taifa na linaogofya kusikia watunga sheria wanaingia ndani ya Bunge wakiwa wamelewa lakini dawa ya tatizo hilo ni kuandaa Taifa katika misingi ya maadili.

Alisisitiza kuwa ili kuwa na Taifa lenye maadili, ni vyema somo la Maadili likaanza kufundishwa tangu shule za msingi ili kujenga jamii yenye maadili mema na hofu ya Mungu. Lema aliwataka Watanzania kuhakikisha wanajenga familia zilizo na maadili na misingi bora ili kuandaa Taifa lenye maadili na hofu ya Mungu.

Museveni amteua Mkewe kuwa Waziri
Wahamiaji haramu 1976 warudishwa nchini kwao.