Mtandao wa wadau unaopambana na unywaji pombe kupita kiasi (TAAnet), leo unaadhimisha siku ya kutokunywa pombe duniani ambayo kwa mara ya kwanza inafanyika kitaifa mkoani Dodoma.

Ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni  “Maendeleo ya Viwanda yataletwa na Udhibiti wa Unywaji Pombe kupita kiasi”

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO),waka 2016 watu zaidi ya milioni tatu wamefariki kutokana na matumizi mabaya ya pombe. Zaidi ya robo tatu ya vifo hivyo vilikuwa ni vya wanaume. Kwa ujumla, matumizi mabaya ya pombe husababisha zaidi ya asilimia tano ya mzigo wa magonjwa duniani.

“Matumizi ya pombe na athari zake ni tatizo linalozidi kukua nchini na linapaswa kudhibitiwa haraka iwezekanavyo. Ongezeko hili la unywaji pombe katika jamii ya Watanzania, TAAnet inazikumbusha taasisi husika pamoja na serikali kuangalia kwa haraka namna ya kudhibiti tabia hiyo ili kunusuru maisha ya vijana yanayoendelea kuharibika kila siku.

“Kama wadau wa kupambana na madhara ya unywaji pombe, tungependa kuona watunga sera wanalitafutia tatizo hili ufumbuzi kwa kuwa na ubunifu ambao utaokoa maisha, kama vile kutokomeza unywaji pombe kupindukia,” ilisema taarifa hiyo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo bado haina sera/muongozo wa pombe ikilingalinishwa na nchi jirani kama Kenya, Malawi huku Uganda ikiwa njiani kumalizia mkakati wa sera yao ya pombe.

Taarifa hiyo ilisema TAAnet inapendekeza kupitiwa kwa sheria na kuweka masharti kuhusiana na matangazo, uuzaji na udhamini wa pombe pamoja na kuonyeshwa kwa onyo la athari za pombe kwenye matangazo ya vilevi ili kupunguza matumizi yake kwa jamii.

“TAAnet inaamini kwamba, endapo kutakuwa na sera ya kudhibiti matumizi mabaya ya pombe, wanaume watawajibika zaidi na kuacha matumizi yaliyopitiliza ya vileo, yanayochangia unyanyasaji wa kijinsia, na badala yake kuchangia ustawi wa familia na kukuza maendeleo kwenye jamii na katika Taifa kwa ujumla.”

Kupunguza matumizi mabaya ya pombe kutasaidia kufikia malengo kadhaa yanayohusiana na afya ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG), ikiwa ni pamoja na afya ya uzazi na watoto, magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukizwa na magonjwa ya akili, majeraha na sumu.

 

Rais Magufuli ampa madaraka Mwinyi
Tuheshimiane, Mavoko amjibu Sallam

Comments

comments