Waziri Mkuu wa Lesotho, Dk. Pakalitha Mosisili  amekubali viongozi waupinzani na baadhi ya maofisa wa kijeshi wanaoishi uhamishoni ambao walikimbia machafuko yaliyotokea nchini humo warejee nchini mwao na kuahidi kwamba atahakikisha wanapatiwa ulinziwa kutosha.

Amesema hayo leo wakati wa kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na wakuu wa nchi wanaounda Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics, Defense and Security Cooperation) kilichofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.

Aidha Dk Mosisili amekubali kutekeleza masharti yaliyowekwa na Wakuu wa Nchi na Serikali na Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC Double Troika Summit), na kuridhia timu ya uchunguzi kwenda nchini humo kufanya uchunguzi wa hali ya kiusalama na kisiasa.

Januari mwaka huu, mkutano wa SADC Double Troika uliagiza ifikapo Februari Mosi, mwaka huu Serikali ya Lesotho iwe imetangaza matokeo ya Tume iliyoundwa kuchunguza matatizo ya kisiasa na kiusalama nchini humo hususani mazingira yaliyopelekea kifo cha marehemu Luteni Jenerali Maaparankoe Mahao ambaye alikuwa Mkuuwa Majeshi.

Naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa akimwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli katika kikao hicho amesema wamepitia ripoti iliyoundwa na timu ya SADC iliyochunguza kuhusu matatizo ya Lesotho ambayo iliwahoji Viongozi wa Serikali, Jeshi, Bunge na familia ya marehemu Luteni Jenerali Mahao.

“Lengo la hatua hizi za SADC ni kuhakikisha inarejesha hali ya amani na utulivu kwenye maeneo ya siasa, ulinzi na usalama katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ili wananchi wake waweze kuishi vizuri,” amesema.

Pia Waziri Mkuu amesema Tanzania inatarajiwa kukabidhiwa uenyekiti wa Wakuu wa Nchi na Serikali na Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC Double Troika Summit), Agosti mwaka huu ambapo kitafanyika kikao kingine nchini  Tanzania.

SADC Double Troika ni kikao maalum kinachojumuisha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na wakuu wa nchi wanaounda Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics, Defense and Security Cooperation). 

 

 

 

 

Mereveille Boppe Awanyamazisha Young Africans
Video: Faulu iliyowamaliza Yanga SC dhidi ya TP Mazembe na 'Highlights' zake (0 - 1)