Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesema licha ya vikwazo haramu vya kimataifa tulivyowekewa, wameweza kudhibiti janga la Uviko-19, katika taifa hilo la kusini mwa Afrika wakati akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Katika siku ya tatu ya Mjadala huo Mkuu (Septyemba 22, 2022), Rais Mnangagwa alisema “licha ya vikwazo hivyo haramu vya kiuchumi tumeweza kutekeleza mkakati wetu wa kitaifa wa kukabili COVID-19 uliotegemea kwa kiasi kikubwa rasilimali zetu za ndani na uwezo wetu wa kitaifa.”

Ameongeza kuwa, hatua ya serikali yake ya kuchukua hatua mapema kabla ya tatizo, imewezesha taifa hili kufikia viwango vikubwa vya utoaji wa chanjo dhidi ya Corona, chanjo ambayo imetolewa pia kwa watoto wenye umri wa kuanzia miaka 12 na kuendelea.

Katika kutekeleza ajenda ya 2030, ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, hususan suala la kumuondoa kila mwananchi kutoka lindi la umaskini, Mnangagwa amesema ushirikiano kati ya Zimbabwe na wadau wake ikiwemo Umoja wa Mataifa ni kipaumbele.

Aidha, amefafanua kuwa “Mathalani katika ngazi ya kaya, miradi ya kuwapatia pembejeo za kilimo, vifaa na usaidizi wa kiufundi, imewezesha ongezeko la uhakika wa chakula katika kaya na kitaifa na hata hivyo ukame wa katikati ya mwaka huu wa 2022 na vimbunga na mvua kubwa vimeleta mtikisiko.”

Vikwazo dhidi ya Zimbabwe, vimewekwa na Marekani, Uingereza na Muungano wa Ulaya na vilianza mwaka wa fedha wa 2001/2002 chanzo chake kikiwa ni Mpango wa marekebisho ya umiliki wa ardhi ulioanzishwa na Rais wa kwanza wa nchi hiyo hayati Robert Mugabe, ambao ulishuhudia kupokonywa ardhi wakulima wachache weupe na ardhi hiyo ikagawanywa kwa raia wa Zimbabwe wasio na ardhi.

Majanga ya afya yametupa uzoefu: Dkt. Mpango
UN: Hakuna dalili ya kumalizika kwa vita Ukraine