Maafisa wa polisi wa kiume, Kaunti ya McDonough nchini Marekani wanakabiliwa na tuhuma za kumvua nguo mtuhumiwa wa kike mweusi akiwa selo.

Kwa mujibu wa taarifa na video za CCTV, mwanamke huyo aliyetambulishwa kwa jina la Ariel Harrison alikamatwa Oktoba 26, 2019 kwa tuhuma za kuendesha gari akiwa amelewa. Imeelezwa kuwa aliondolewa kwenye gari lake na kuwekwa kwenye gari la polisi kabla ya kufikishwa kituoni, lakini hakuwa amefungwa pingu.

Bi. Harrison ambaye ni mlemavu wa jicho moja alishtakiwa kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa, na hukumu yake inatarajiwa kutolewa Agosti 10 mwaka huu. Lakini video iliyopatikana hivi karibuni huenda ikabadili hali ya mambo.

Mwanamke huyo anasimulia kuwa hakuwa ametumia kilevi cha aina yoyote na kwamba kadiri alivyojaribu kuwaeleza askari hao walioongozana na askari mmoja wa kike, hawakutaka kumsikiliza na hata hawakumpima ulevi kwa kifaa maalum walichokuwa nacho.

Bi. Harrison mwenye umri wa miaka 31 ambaye pia ni watoto watatu, anasema kuwa alipofika katika selo hizo, polisi hao walikuwa wakimpiga na kifaa cha kutetemesha (taser) mara kadhaa.

Video ya CCTV Camera iliyotelewa hivi karibuni inaonesha askari wawili wa kiume wazungu wakimvua nguo zote Bi. Harrison kwa madai kuwa alikataa kuvua nguo mwenyewe ili apewe nguo maalum. Ripoti iliyotolewa imeeleza kuwa mwanamke huyo aliwaomba sana wasifanye hivyo huku akiwaonya kwa unyanyasaji wa kingono, lakini hawakusita.

Bi. Harrison anasema kulikuwa na askari mmoja wa kike na alimwambia mara kadhaa kuwakataza askari hao wa kiume lakini naye pia aliwaunga mkono.

“Niliwaambia hii sio sahihi. Hiki sicho mlichopaswa kufanya, hawa askari wa kiume hawakupaswa kuwa hapa wakati nabadili nguo. Yule askari wa kike aliniambia ‘wako hapa na mimi’. Kwa ufupi hakujali, nilijisikia kudhalilishwa,” Bi. Harrison anasimulia.

Anaeleza kuwa askari mmoja alimshika miguu yake na askari wawili wa kiume walimvua nguo kwa nguvu. Kisha walimuacha akiwa mtupu ndani ya selo hizo, kabla ya kumpa nguo maalum.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa askari hao walipotakiwa kujitetea, walisema walimvua nguo kwakuwa hakuwa anatoa ushirikiano.

Video ya tukio hilo iliibuliwa na wanaharakati za haki za wanawake, ‘Women of Mcdonough County (DWMC)’ kwa msaada wa Freedom of Information Act (FOIA).

DWMC wameendelea kukusanya michango ya kumsaidia Bi. Harrison kuendesha kesi dhidi ya maafisa waliomdhalilisha akiwa selo. Pia, wameanzisha harakati za kuitaka Serikali ya Kaunti hiyo kuwaondoa maafisa hao katika utumishi wa umma mara moja; na kuondoa mashtaka dhidi ya Bi. Harrison.

Martinez aibeba Argentina Copa America 2021
TB Joshua: Chanzo cha moto kuzuka kanisani wakiomboleza chaanikwa