Nahodha na mshambuliaji wa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona Lionel Messi, amempinga mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo Eric Abidal, kufuatia kauli aliyoitoa siku za karibuni kwa kudai wachezaji walikua wanacheza chini ya kiwango chini ya utawala wa aliyekua meneja klabuni hapo  Ernesto Valverde.

Meneja Valverde alifutwa kazi mwezi uliopita (Januari), na nafasi yake tayari imeshajazwa na Quique Setien, aliyetokea Real Betis.

Abidal, ambaye alicheza sambamba na Lionel Messi, alinukuliwa na gazeti la michezo la Hispania la Diario Sport akitoa madai hayo, baada ya kuulizwa kiwango cha timu wakati wa utawala wa kocha Valverde.

Katika taarifa iliyotolewa kwenye gazeti hilo Abidal alinukuliwa akisema: “Wachezaji wengi walionyesha kubweteka na kujikuta wakicheza chini ya kiwango, jambo ambalo lilidhihirisha mapungufu mengi kwenye kikosi chetu.”

“Mahusiano ya meneja na wachezaji yalionekana kutokua mazuri, kufuatia kilichojidhihirisha uwanjani. Nililazimika kuushauri uongozi kutafuta mbinu mbadala ambazo zingeweza kuisaidia timu, na ndipo maamuzi ya kutimuliwa kwa Valverde yalipoanza kuchukua mkondo wake.”

Lakini jana jumanne Messi, mwenye umri wa miaka 32, alijibu tuhuma hizo kwa kusema:  “Unapoamua kuzungumzia wachezaji, unapaswa kutaja majina, sio kuwajumuisha wote na kuwaingiza kwenye tuhuma za kucheza chini ya kiwango, haipendezi kufanya jambo kama hilo kupitia vyombo vya habari.”

Messi amesema meneja Valverde aliondolewa klabuni hapo wakati FC Barcelona ikiwa inaongoza msimamo wa ligi ya Hispania (La Liga), na ameshangazwa kwa tuhuma wanazotupiwa wachezaji.

“Nazungumza kutoka moyoni, sijapendezwa na jambo hili, ni bora mtu akajali nafasi yake kwa kusema ukweli na sio kuzungumza eti kwa sababu unaongeza na chombo cha habari kilichotaka kufahamu nini tatizo lililopelekea kuondoka kwa meneja aliyepita.” Alisema Messi ambaye mwishoni mwa mwaka jana alifikisha idadi ya tuzo sita za mchezaji bora wa dunia (Ballon d’Or).

“Wachezaji wanafahamu majukumu yao wanapokua uwanjani, na ndio maana kila mchezo tumekua tunajitahidi na kutoka uwanjani tukiwa na matokeo mazuri, ni mara chache sana inatokea tunapoteza, lakini bado kiwango kinaonekana kuvutia.”

Abidal alicheza kikosi kimoja Lionel Messi kuanzia mwaka 2007 hadi 2013, na baadae aliondoka klabuni hapo na kurejea nyumbani kwao Ufaransa kujiunga na AS Monaco, mwaka mmoja baadaye alitimkia Ugiriki kuitumikia Olympiacos.

Juni 2018 alirejea FC Barcelona na kutangazwa kuwa mkurugenzi wa michezo, akichukua nafasi ya Roberto Fernández aliyefanya kazi hiyo tangu mwaka 2014.

Serikali yalifungia kanisa la Asembles of God Moshi
“Moi alikuwa na sura mbili,” Mpinzani asimulia alivyobishana naye kwenye mkutano